Advertisements

Balaa alilianzisha kwa masister pale St. Mary’s RC primary school, bahati iliyoje kumlea mtoto mwenye kipaji kikubwa cha soka kama kile. Baadaye alisogea Cardinal Langley Roman Catholic high school kuzishangaza rosari za mapadri waliokubali kuvua miwani wamuone vema akisata kabumbu. Mtoto fulani kutoka Ireland aliyeichagua Uingereza ili awafundishe mpira.

Alianza kukipiga Manchester United akiwa na miaka 12 tu. Alisusia mazoezi ya timu ya shule ili awahi pale Leigh sports training complex kujifua na watoto wa Lee Sharp, academy ya Manchester United. Aliwahi ili akawaoneshe tofauti ya mpira wa shule na mtaani. Mtoto Paul scholes fundi dimbani, mtoto Paul Scholes mhuni mtwangwa buti. Alipata nafasi ya kujiunga na United ya watoto akiwa na miaka 14.

Advertisements

Babu Fergie alimpokea Scholes kwenye timu ya wakubwa 1994, alimpokea striker aliyefunzwa kuua nyavu kwenye timu ya watoto ila miwani ya Fergie ilimuona kwa sura tofauti. Uimara wake wa kupiga pasi, ukabaji wa kikatili, janjajanja nyingi akiwa hana mpira, babu alitazama juu kumsemesha Mungu, nitakulipa nini mimi kwa kuniletea kiungo niliyemuota miaka yote.

Babu alimtumia kwenye mechi zaidi ya 700 katika dimba la kati. Alichombadilisha tu ni eneo. Siku akimpanga kiungo mkabaji, mabeki wanapewa likizo, kazi zote anazimaliza kabla hazijafika kwao. Siku ya Kiungo mchezeshaji, mastraika wana maswali ya kujibu kwanini wamekosa magoli mengi hivo. Siku nyingine anaamua kuwapa mateso ma fullback wa wapinzani, anamchezesha kiungo wa pembeni. Paul Scholes “a versatile player”.

Advertisements

Scholes pasi? Alipiga pasi yake kichwani kwanza, alafu moyoni kisha mguuni. Scholes shuti? Shuti la mita 20 angepiga kwa nguvu ya mita 40 alafu bado angelenga lango. Siku akihitajika acheze box to box yeye angecheza goal to goal. Scholes rafu? Mpira wa kuchukua kawaida tu angekupa mwili kwanza alafu akukanyage ndio aondoke.

Binadamu mmoja Socrates kutoka Brazil anaamini Scholes alistahili kucheza Brazil, Zinedine Zidane anaamini Scholes ndiye kiungo mgumu kuwahi kumkabili. Thiery Henry anaamini Scholes ndiye mchezaji bora wa epl miaka 20 iliyopita.