Advertisements

Hofu imetawala jangwani baada ya wachezaji wao kupata majeraha mfululizo huku wakikabiliwa na michezo migumu mbele yao.

Mapinduzi Balama ambaye aliumia kifundo cha mguu akiwa mazoezini, Pappy Tshishimbi akisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja pamoja na Haruna Niyonzima akiumia katika mchezo dhidi ya Biashara United juzi kumeifanya klabu ya Yanga kuingiwa na hofu namna gani wataikabili michezo iliyopo mbele yao.

Yanga ina kibarua kikubwa dhidi ya Kagera Sugar itakayokipiga katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba huku Jumapili ikitakiwa kumalizana na Simba SC katika mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho (FA) utakaopigwa uwanja wa Taifa.

Akizungumza na Mwananchi Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesema kuwa kuumia kwa wachezaji wake nyota ni pigo kubwa sana kwa klabu ya Yanga lakini hana jinsi zaidi ya kukubaliana na hali iliyotokea.

“Inaumiza lakini hakuna jinsi zaidi ya kukubaliana na hili linaloendelea Tshishimbi mgonjwa, Balama mgonjwa na Niyonzima naye hivyohivyo” alisema

“Kukosekana kwa Niyonzima itakuwa pigo kutokana na uwezo wake uwanjani na pia ni mchezaji nyota katika kikosi cha kwanza na hilo linajulikana, lakini ngoja tuone inakuwaje kwa upande wa afya yake” aliongeza.