Klabu ya Yanga SC leo imetoa maamuzi ya kumkata mshahara wa Tsh 1,500,000 mchezaji wa klabu hiyo Bernard Morrison kutokana na makosa aliyoyafanya klabuni hapo, ambayo klabu imetambua kama ni uhujumu na uvunjifu wa taratibu na kanuni za klabu hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa leo na klabu ya Yanga SC kupitia Kaimu Katibu Mkuu wao Wakili Simon Patrick

Katika barua iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo klabu hiyo imesema kuwa imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na mchezaji wao cha kuitisha na kufanya mahojiano na chombo cha habari bila kufuata utaratibu uliowekwa na klabu hiyo

Aidha barua inaeleza kuwa mchezaji huyo alishaelezwa taratibu zilizowekwa na klabu hiyo na akaamua kuziuka taratibu hizo akiwa na nia ovu, hivyo klabu imeamua kutoa adhabu ya kumkata mshahara Morrison.

Pia klabu ya Yanga SC imetoa wito kwa wachezaji wake na umma wote kutambua kuwa ndani ya klabu hiyo hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya klabu na haitavumilia utovu wa nidhamu utakaofanywa na mchezaji yeyote.

#Sign Up for More