Dunia inamfahamu Harry Houdini kama mtu mdanganyifu sana tena mwenye maajabu mengi mno kutokana na uwezo wake wa kutoroka katika kila gereza alilofungwa pia kufanya maajabu yaliyoshangaza ulimwengu.

Siku moja Houdini alitangaza kuwa hakuna gereza lolote linaloweza kumfunga na akashindwa kutoroka ndani ya dakika tu kwasababu yeye ndiye mkuu wa maajabu ulimwenguni.

Basi kama ilivyo ada Houdini alipokea mwaliko wa kuingia gerezani kisha afungiwe humo na aaze maajabu yake na kujitoa mwenyewe, kwa majigambo zaidi aliingia ndani ya chumba cha gereza akiwa amevaa nguo za kiraia, huku pingu zikiwa zimefungwa mikononi mwake kisha mlango ukafungwa!.

Houdini kwa imani thabiti akafungua mkanda kiunoni mwake na kutoa kipande chembamba cha waya wa chuma kilichoonekana kuwa na nguvu sana kisha kwa madaha akaanza kazi ya kufungua kufuri la mlango wa gereza taratibu kabisa.

Dakika moja ikapita, ikawa bado Houdini hajafanikiwa kufungua mlango wa chumba kile, nusu saa ikapita na muda ukazidi songa hatimaye saa moja ikapita Houdini bado hakufanikiwa kufungua mlango ule!.

Mwili wa Houdini ukalowa jasho akili yake ikavurugika, alichoka kabisa hakujua ni wapi amekosea mpaka ameshindwa kufungua mlango ule kwa dakika moja tu.

Hatimaye masaa mawili yakapita Houdini akiwa ndani ameshindwa kufungua mlango, ujuzi wake wote na maajabu yake yote vilishindwa kufanya kazi kabisa.

Baada ya kuchoka, hofu na mashaka Houdini alidondoka chini huku akiegemea mlango wa gereza, bila kutegemea mlango ukafunguka na Houdini akaja kutolewa akiwa hajielewi na amelowa jasho mwili mzima.

Ukweli ni kwamba mlango ule haukufungwa kwa kufuri kama ambavyo Hioudini alikuwa akiwaza alipokuwa anaingia ndani ya chumba kile, Bali mlango ule ulifungwa ndani ya ufahamu wa akili ya Harry Houdini mwenyewe.

Houdini alianza kufungua mlango bila kuangalia mlango ule umefungwaje, hadithi hii inaweza kufanana pia katika maisha yetu ya kila siku.

Mara nyingi kuwa na papara papara juu ya jambo fulani bila kuchunguza huweza kutuingiza katika matatizo na tukashindwa kujikomboa kabisa…

MAAMUZI YAKO LEO, NDIYO MAISHA YAKO YA KESHO…

Mimi naamini kuwa moja kati ya mambo yatakayoweza kukupa ujasiri wa kufanya maamuzi mazuri ni UHURU WA FIKRA kwa kutambua ukweli na mahitaji yako katika maisha.

Picha iliyopo hapo juu inamuonesha bwana mmoja ambaye aliyeko gerezani na badala ya kuchagua funguo itakayomuweka huru anaamua kuchagua chakula.

Ukweli ni kwamba si vibaya kuchagua chakula ambacho atakula na kitamshibisha, lakini JE? anatambua thamani ya kile anachoacha kukichagua? JE chakula kinaweza kumfanya awe huru na maisha yake?.

Penginepo amekata tamaa kabisa na kuona kuwa gerezani ndiyo mahali sahihi kwa wakati huo, lakini si kweli kwani hata Biblia Takatifu katika kitabu cha Yohana 8-32 kinatuambia kuwa

Nanyi mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru ninyi

Bwana huyu anaweza kusaidiwa kwa kupatiwa uhuru wa fikra ambao unaweza kufungua mawazo yake na kutambua kweli ambayo itamuweka huru.

Huyu naye ni sawa na Harry Houdini pamoja na watu wote ambao wamefungwa katika fikra/fahamu zao na wanashindwa kutafuta iliyo kweli na itakayowafanya kuishi huru.

Watu kama hawa wanahitaji msada wa karibu sana, ili kuwakomboa…

Processing…
Success! You're on the list.