Ole Gunnar Solskjaer, Kocha mkuu wa Manchester United amekiri kuwa kiungo wake Paul Pogba ni miongoni mwa wachezaji bora duniani kutokana na uwezo anaouonesha akiwa uwanjani.

Pogba kiungo mwenye umri wa miaka 27 aliwashangaza wengi kwa umahiri aliouonesha katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham kwa kutimiza majukumu yake vema na kuhusika kwenye pointi moja ambayo waliipata Manchester United baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1.

Akitokea benchi kati ya dakika ya 63 huku United ikiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya Tottenham inayonolewa na Jose Mourinho, bao hilo lilifungwa dakika ya 27 na Steven Bergwijn.

Bao la kusawazisha majonzi ya United liliwekwa wavuni kati ya dakika ya 81 na Bruno Fernandez kwa mkwaju wa penati ambayo ilisababishwa na Paul Pogba baada ya kuchezewa faulo ndani ya box na Eric Dier.

Sare hiyo inawafanya United kufikisha point 46 wakiwa nafasi ya tano mbele ya Tottenham wenye pointi 42 nafasi ya nane, huku wote wakiwa wamekamilisha michezo 30

“Kipindi cha pili kwa namna ambayo tumecheza tulistahili kupata pointi tatu lakini hamna tatizo tumeanza vizuri wachezaji wangu wamecheza vizuri Pogba amefanya makubwa na ni mchezaji bora ulimwenguni kwa sasa kwa kuwa ana vitu vingi. alisema Ole Gunnar.