SEHEMU YA TANO

Ilipoishia…

Alimwaga mafuta mahali pote kisha akawasha moto paliteketea na hakuna ushahidi wowote ulibaki, baada ya kazi ile kumalizika alielekea ndani ya gari yake akatoa kisanduku kile na kukiweka kwenye  siti kisha akawasha gari na kuondoka.

Sasa endelea…

Usiku wa manane nilishtuka kutoka usingizini, nilijikuta nimelala kwenye kitanda kikubwa, kizuri sana sijawahi kulalia tangu kuzaliwa kwangu niliogopa kidogo chumba kiikuwa kimepambwa wa nakshi nzuri na harufu nzuri ilitawala chumba kile.

Nilihisi kama vile nimepaa kwenda peponi sikujua ni wapi pale nilikuwapo, nilijitahidi kukumbuka nimefikaje kitandani pale lakini hakuna kitu niliweza kukumbuka, nilijifunua shuka na kutoka kitandani.

Looh..!! nilishangaa kukuta nimelala na nguo zangu zilezile ambazo nilikuwa nimetoroka nazo, nilitoka nje sebuleni nilshangaa kumkuta black akiwa kifua wazi anatazama mpira kwenye televisheni.

Nilishuka ngazini nikaenda kujumuika naye alinikaribisha mahali  pale, tulikaa kwa dakika chache kisha nikamuomba anioneshe maliwatoni niende kujifanyia usafi wa mwili.

Alinisindikiza mkapa bafuni na kunielekeza jiinsi ya kutumia bafu na maji ya bomba.

Hakika moyoni mwangu nilijuwa kuwa ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuoga ndani ya beseni vile tangu niuingie utu uzima, maji yenye ya vuguvugu, nilioga huku mawazoni mwangu nikiwaza mambo mengi hasa safari yangu ya Dar jinsi ilivyoharibika ghafla.

Nilioga chapu kisha nikatoka bafuni na kuelekea chumbani kwangu, nilikuta nguo nzuri za kulalia zikiwa ndani ya kabati, nilijifuta maji kisha nikakausha mwenye zangu kwa mashine.

Mezani niliona vipodozi vya kila aina vingi ambavyo nilivipenda, moyoni mwangu nilijiuliza kama kulikuwa na msichana aliyekuwa anaishi katika chumba hicho au lah! Au Black alikuwa ameoa

Nilipaka mafuta vizuri baada ya hapo nikatoka kwenda sebuleni, nilimkuta Black bado akiwa anaangalia mpira nikaona vyema niende nikakae nae tu.

Nilipokuwa nikishuka ngazi aliniangalia sana mpaka nikaanza kusikia uoga, moyoni mwangu nilianza kuwa na maswali mengi kwanini ananiangalia sana vile.

“karibu Suzana…. !! jisikie salama kabisaa…” aliniambia huku akiwa anatabasamu..

Baada ya kuketi ilibidi nimuulize nimelala tangu saa ngapi, nilishangazwa aliponiambia kuwa nilianza kulala kwenye gari hadi nilipofika hapa nyumbani bado nilikuwa nimelala hivyo walinibeba yeye na Faraji kisha wakanilaza kitandani na ule muda nimeamka ulikuwa ni saa saba usiku.

Nilishangazwa na maelezo yake nimewezaje kulala muda wote huo yaani tangu asubuhi mpaka usiku wa manane ooh!!.. Blackm aliinuka na kuleta chakula, tukaanza kula kwa pamoja huku tukiangalia mpira.

“Suzana… mbona tuliporudi hatukukuta ulienda wapi…?” Black aliniuliza.

“Black nilirudi kutafuta kisanduku changu, nafikiri nimekidondosha wakati tukiwa tunakimbia..” nilimjibu huku machozi yakinilengalenga.

“dah pole sana Suzana… tutafanyaje sasa ili kukipata tena…” Black aliuliza tena

“Sijui cha kufanya black…. sielewi nitajuaje mambo yaliyopita bilia kile kisanduku aah…”

“Usijali Suzana tutajaribu kukitafuta naamini tutakipata usijali mama…” Black alinieleza

Baada ya kuniambia hivyo nilimuona akipiga magoti chini huku machozi yakichuruzika mashavuni mwake nilimuona akinyanyua mdomo wake na kunambia

“Hello Suzana… mimi ni mtu mbaya sana, nimefanya kazi za uovu ili kupata pesa… hatimaye nina kila kitu ninachokihitaji maishani mwangu… lakini bado nahisi sijatimiliwa..” Black aliniambia

“Suzana nimewakosea watu wengi sana, lakini leo hii nataka nikuombe msamaha wewe kwani hao wengine bado siwezi kuwapta kwa mara moja,  tafadhali nisamehe Suzana… mimi ni mkosefu mbele zako!!”  aliniambia maneno ya uchungu huku akiwa amepiga magoti ba machozi yanamtoka..

“Nimeamua kubadilika Suzana  sitaki tena kuishi maisha yale… nilishapanga kuacha maisha haya ya uovu, lakini barua aliyoiandika mama yako imenipa ujasiri wa kuacha kabisa, na kutamani kusafisha moyo wangu..” Black aliendelea kuongea maneno ya uchungu na majuto hakunipa hata nafasi ya kuongea jambo.

Nilijikuta nikiacha chakula na kushuka chini, nikamkumbatia Black bila hata ya kujielewa akilini mwangu nilijiuliza barua aliyoiandika mama yangu yeye ameiona wapi?, ni kweli ameamua kubadilika na kuwa mtu mwema baada ya kufanya uovu wote huo.

Ni kweli amenisaidia kutoka katika shida zile zote je hiyo pekee haitoshi kumuamini black na kumpa nafasi nyingine kama binadamu wa kawaida?

“Black samahani…. “ .

“Bila samahani Suzana..”

“Kwanini unaitwa black na jina lako kamili  ni nani..”

“Jina langu kamili ni Kelvin…. KELVIN DANIEL.. Jina la black nilipewa kama jina la siri ili nisiweze kutambulika…”

“sawa naitwa Suzana… SUZANA HERMAN..  abiria ambaye nilitekwa, nikaokolewa na mtekaji aliyemua kuwasaliti wenzake na kuwa msamaria mwema…”

“Kelvin nimekusamehe kwa yote kama vile Mungu alivyotufundisha.. ila jambo moja  nakuomba fanikisha kuokoa abiria wale ambao wametekwa… ukifanya hivyo Mungu atakusamehe yote yaliyopita…”

“Suzana… tayari vita hiyo nimeshaianza, nilimkabidhi rafiki yako Jimmy simu pamoja na  kipande cha nguo yako naamini atanitafuta tu..”

Moyo wangu ulijawa na furaha baada ya kusikia hivyo, sasa nilianza kumuangalia Kelvin kama Kelvin mtu ambaye amenikomboa kutoka mateka na sio Black tena mtu ambaye alishiriki kuniteka nilimkumbatia Kelvin na kumshukuru kwa jambo lile.

Kelvin aliniinua na knipeleka chumbani aliniomba nipumzike na mambo mengine zaidi tungeongea siku iliyofuata.

Alipokuwa akitoka chumbani kwangu nilimuangalia kwa umakini, moyoni mwangu nikajisemea “kumbe hata wanaume nao huwa ni wazuri hivi…” ukiachana na uovu wote aliofanya Kelvin alikuwa ni kijana mzuri sana, mwili wake ulijengeka vema na rangi yake ya weusi ilimfanya kuonekana shababi wa ukweli..

                              *************************************

Ngriiiiiiiii ngriiiiiiiiiiiiii….. muito wa simu ulimshtua Kelvin (black) kutoka usingizini, aliangalia namba na mapema alitambua ni nani anapiga, akapokea haraka haraka,

“Hello Serena…”

“Black… ni mimi Serena, nahitaji msaada wako..” Jimmy aliongea kwa kutumia jina la Serena kama alivyoambiwa mwanzo.

“Naam nakusikiliza Serena… nini unahitaji kifanyike..? Kelvin aliuliza

“Nisikilize Black… nimewasikia wakuu wakiongea kuwa tunakaribia kufika mpakani mwa Tanzania na Malawi…?

“Tafadhali naomba msaada wako Black kwani tukishavuka mpakani itakuwa vigumu kutuokoa..”

“Sawa Jimmy nimekuelewa… unafikiri kwa makadirio ni kwa muda gani..? Kelvin aliuliza

“Nimewasikia… wa—- ma itachuku— matatu..”  Jimmy alisema

Simu ilianza kusumbua kutokana mtandao kupatikana kwa shida, Kelvin alisikia matatu… hakujua ni masaa matatu au laah, alinyanyuka kitandani pake kisha akapanga mbinu za kuwaokoa Jimmy na wenzake.

Kelvin alitoka nyumbani na kumuacha Suzana akiwa bado amelala, alielekea hadi kituo cha  kituo cha polisi kikubwa pale Morogoro  na kujitambulisha kwa jina la KELVIN NYERERE, kisha akatoa taarifa pamoja na uthibitisho,

Kelvin aliamua kubadilisha jina lake ili isije ikawa shida hapo baadae, japo alienda kutoa taarifa zote lakini aliogopa kuwa isije kesi ikaja kumrudia yeye mwenyewe kwani naye ni miongoni mwa watekaji wa mabasi.

Haraka simu ilipigwa mpaka makao makuu ya polisi kitengo cha upelelezi jijini Dar es salaaam. Na taarifa zote zikatolewa, zikiambatanishwa na namba ambayo ilitumika kufanya mawasiliano.

Kelvin aliambiwa kubaki polisi mpaka hapo zoezi zima litakapokamilika, kitengo cha upelelezi kilifanya kazi ya kuitafuta namba ile  kwa njia ya GPS hapo wakagundua kuwa watu hao wanakaribia kuvuka mpaka wa Tanzania kuingia Malawi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Omari Mkorowine aliagiza kikosi cha askari kumi ambapo watano walitoka katika kikosi cha upambanaji watatu katika kikosi cha msalaba mwekundu na wawili kutoka katika kikosi cha upelelezi.

IGP Mkorowine na askari kumi walipanda helikopta na kuelekea mpakani mwa Tanzania na Malawi, alifanya hivyo kwani alijua kuwa angepiga simu huenda vibaraka walioweka mpakani hapo wangetoa taarifa kwa watekaji hao, na hatimaye wangewakosa.

Operesheni ya uokozi ilipachikwa jina la Operesheni Te-samaria na ilipangwa kufanyika kwa muda wa dakika kumi na tano tu, ndani ya Tanzania kabla watekaji hawajavuka mipaka kwani kuendesha operesheni nje ya mipaka yako ingekuwa ni hatari kwa jeshi la polisi la Tanzania.

IGP Mkorowine akiongoza kikosi cha askari kumi walitua katika msitu uliokaribu sana na  ofisi za mpakani mwa Tanzania na Malawi mahali ambapo magari yote hupitia kwa ajili ya ukaguzi.

Baada ya dakika chache waliona malori mawili yakiwasiri pale mpaka, IGP alitoa ishara kwa askari wake kujiandaa kwa uvamizi, kabla ya kufanya hivyo alipiga simu makao makuu ya polisi na kuwaomba wapiga simu mpakani na kuwaeleza kuwa IGP atakuwa hapo muda mfupi ujao.

Alifanya hivyo kwani tayari alishaona malori ambayo walitakiwa kuyakamata, hivyo hata kama vibaraka wangehitaji kutoa taarifa kwa watekaji wangekuwa tayari wameshachelewa.

Saa hiyohiyo IGP alijitokeza msituni na askari wake ambao walikuwa wameshajipanga kukabiriana na lolote litakajiri.

Walifika na kuwaweka chini ya ulinzi baadhi ya watekaji ambao walikuwa katika lori la pili, baada ya kuona hivyo walengaji walioko lori la kwanza waliwasha lori na kutaka kukimmbia hivyohivyo wakielekea msituni ambako ndiko waliona wangeweza kujificha.

Ghafla watekaji walianza kufyatua risasi kwa polisi ambao walikuwa wamejificha katika kichaka, amri ilitolewa na askari polisi kujibu mashambulizi ya risasi.

Ndani ya dakika kumi watekaji wanne walipoteza maisha katika majibizano ya risasi, waliobaki waliamua kusalimu amri baada ya kuona wamezidiwa na hawana ujanja tena.

IGP mwenyewe alifungua malori yale kisha wakatoa mizigo ambayo ilikuwa imepangwa ili kuwaficha mateka,  baada ya zoezi ilo mateka wote walikombolewa wakiwa salama.

IGP aliangalia saa yake ya mkononi na aliona operesheni yake imekamilika ndani ya dakika kumi na mbili, alifurahi kufanikisha haya yote na askari wake wakiwa wazima kabisaa.

Hali za mateka hazikuwa nzuri, watoto walikuwa wamedhoofu mno, watu wote waliishiwa nguvu kwa kupata hewa ndogo.

Ililetwa helikopta nyingine kwa ajili ya kuwapakia mateka na kuwarudisha jijini Dar es salaam ambako ndiko makao makuu ya Polisi.

Mahojiano kati ya polisi na abiria yalianza, kila abiria alitoa maelezo yake kwa umakini Jimmy alihojiwa katika chumba maalumu alieleza jinsi safari ilivyoanza mpaka walivyotekwa na kukombolewa.

Aliulizwa kuwa alipata wapi simu ambayo aliitumia katika kufanya mawasiliano na Kelvin, Jimmy alifikiri kwa muda kisha akaanua kusema kuwa simu ile aliificha wakati wa ukaguzi hivyo aliingia nayo ndani ya kambi ya watekaji na alipopata nafasi ndipo aliamua kumpigia rafiki yake kwa ajili ya kuomba msaada.

Aliulizwa kama aliweza kutambua sura ya mtekaji wowote, alifikiri kwa muda kisha aliomba karatasi na penseli, alipatiwa vifaa hivyo ndipo akaanza kuchora sura ya Mr Herman ambayo ndiyo sura aliyokuwa anaikumbuka kw wakati huo.

Alitumia dakika ishirini kuichora sura hiyo na kuipaka rangi, wataalamu wa utambuzi wa sura kwa mtandao wakaichukua na kuingiza katika mtandao.

Waliifanyia utafiti na hatimaye waliipata picha ile ilitumwa kwenye hoteli ambayo mtuhumiwa Mr Herman alianzia safari yake, walifanya ulinganisho wa picha ile pamoja na picha ambayo ilipatikana kutoka kwenye CCTV camera za hotelini hapo, ilifanana kwa asilimia 99.9.

Serikali ilijiridhisha kwa uchunguzi wao kuwa Mr Herman ndiye muhusika mkuu wa uhalifu unaohusisha kuteka na kuuza binadamu.

Hivyo ilitoa amri kwa vikosi vyote nchini kumtafuta mtu huyo mahali popte alipo, pia serikali ilishangazwa   kumkuta  mhalifu ambaye walikuwa wakimtafuta kwa muda mrefu, palepale mpenzi wa Faraji alikamatwa kwa kosa la kuuza madawa ya kulevya.

                            ********************************************************

Baada ya zoezi zima la ukombozi kukamilika jeshi la polisi lilimuachia huru Kelvin na kumuambia aende nyumbani akaendelee na shughuli za kujenga taifa.

Kelvin alirudi nyumbani kwake ikiwa yapata saa tatu asubuhi, aliingia ndani na kumkuta Suzana tayari ameshaandaa chakula cha asubuhi.

Kelvin alimsimulia Suzana jinsi alivyofanikisha zoezi zima la kuwakomboa Jimmy na wenzake alimwambia kuwa ale chakula haraka kisha waanze safari ya kuelekea Dar es salaam.

Suzana hakutaka kuchelewa kabisa, alijianda haraka kisha wakapanga safari ya kuondoka Morogoro kuelekea Dar es salaam.

Kelvin alipiga simu kwa rafiki yake Faraji na kumpa pole kwa kukamatwa kwa mpenzi wake, pia alimuambia kuwa anasafiri anaenda mbali sana na asingeliweza kurudi punde.

Baada ya simukukata simu ya Faraji alipiga tena simu  kwa Jimmy kisha akamueleza kuwa wanakuja Dar kwa ajili yake, hivyo akae kitako kuwasubiri. Jimmy hakuwa na mahali popote pa kufikia hivyo Kelvin aliamua kumuunganisha Jimmy kwa marafiki zake ambao walikuwako Dar es salaam, kisha aliwaomba wampeleke Jimmy hotel ya Serena kwa mapumziko mpaka pale wao watakapowasiri.

Haukupita muda mrefu wakawasili viwanja vya ndege vya Dar es salaam, walichukua tax na kuelekea moja kwa moja katika hoteli ya Serena, moja kati ya hoteli kubwa sana Dar es salaam.

Kwa mara nyingine tena bila ya kutegemea Suzana aliuona uso wa Jimmy alikimbia huku akifurahi na kumshukuru Mungu akamkumbatia Jimmy.

Wote walibaki wakitokwa na machozi ya furaha, Kelvin alisimama kando akiwaangalia tu, hakuwa na la kufanya japo taratibu moyo wake ulianza kumpenda Suzana, alianza kutamani aishi nae kama mpenzi wake ila alijua kuwa amechelewa kwani Jimmy alikuwa na nafasi kubwa sana ya kuushinda moyo wa Suzana.

Walisalimiana kisha wakaingia katika chumba kimoja ili wazungumze kwa urefu na mapana, furaha ya Suzana ilirejea tena upya alijihisi yupo katikati ya mashujaa wawili waliosaidia kuokoa uhai wake.

Jimmy alimueleza Suzana jinsi alivyosaidia na Kelvin mpaka kufikia pale, kisha alikitoa kipande cha nguo ambacho Suzana alimpatia Kelvin, alikirudisha kwa Suzana na kumshukuru kwa uwezo wake wa kutunza ahadi mpaka ameitimiza na sas yeye yuko huru.

Jimmy aliwaambia kuwa ilikuwa ni ndoto yake kufika Dar es salaam, ijapokuwa amefika ila kwa misukosuko, alisisitiza  kuwa bado ndoto zake za kuwa mwanamuziki zimebaki palepale na bado hilo atalikamilisha

“Jimmy una ndugu yeyote hapa Dar…” Kelvin aliuliza

“Hapana sina ndugu yoyote lakini nitapambana tu…” Jimmy alijibu..

Mchana ule waliongea mambo mengi sana walikaa hotelini pale muda wote wakifurahi, japo akilini mwake Suzana aliamini kuwa tayari ameshapoteza siri alizotakiwa kuzifahamu kuhusiana na familia yake,  hasa kaka yake.

Kelvin hakumwambia Suzana jambo lolote kuhusiana na kile ambacho alikisoma kutoka katika kisanduku chake, aliogopa asije kuulizwa kwanini alifungua kitu ambacho hakikumuhusu.

Walikaa hotelini pale mpaka usiku ulipoingia, Kelvini alienda kupangisha vyumba vitatu kwa ajili ya kujipumzisha wote watatu.

Wakiwa chumbani mwao wanakula chakula Kelvin aliamua kuwasha televisheni ili waangalia habari na nini kinaendelea katika uchunguzi unaofanywa na jeshi la polisi.

Pamoja waliangalia habari huku wakipata chakula cha usiku, wote watatu walipigwa na bumbuwazi!! baada ya kuona picha ya Mr Herman ikitangazwa kuwa ni mhalifu anayehusika na utekaji na uuzaji wa binadamu nchi za nje na tayari ameshatiwa mikononi mwa jeshi la polisi.

Suzana ndiye ambaye alishangazwa zaidi baada ya kusikia aliyekamatwa anaitwa Eric John Herman, mzaliwa wa Bumbuta, Dodoma aliyekuwa akiishi Morogoro.

Kelvin na Jimmy waligundua kuwa Suzana hakuwa sawa baada ya kusikia habari zile, walishangaa kwanini wakati wao walitegemea kukamatwa kwa mtu ambaye aliwateka kungekuwa furaha kwa Suzana.

Suzana aliinuka mahali alipokuwa amekaa, akaenda kuzima televisheni hakutaka tena kuangalia, aliporudi kitini alimuomba Kelvin kuwa kesho anataka kwenda kuonana na yule mtekaji aliyekamatwa.

Kelvin hakuwa na kipingamizi kwa ombi lake japo alimuomba kuwa yeye hasingeweza kumsindikiza mpaka polisi kwani kufanya hivyo kungehatarisha usalama wake alihofia huenda nayeye angekamatwa.

Usiku ule haukupita vizuri Suzana alibaki na mawazo ambayo alishindwa kuamini kuwa ni kweli au anaota tu, Kelvin alimbembeleza Suzana aseme ni nini kilimsibu, hakujibu badala yake alimwambia nahitaji kulala kila kitun kitajulikana kesho asubuhi.

Basi hakuna tena aliyejaribu kwenda kumbuguzi Suzana, waliamua kumuacha aendelee kulala tu kisha Kelvin na Jimmy wakarudi Sebuleni kuendelea na maongezi yao.

“Jimmy… natamani niu..lize jambo kwakoo.. kuhusiana na Suzana..” Kelvin alisema

“Bro… Kelvin najua umeshaanza kumpenda Suzana… nafahamu hilo..” Jimmy alijibu

“aah usijali bro.. ni kweli.. lakini kama ni mpenzi wako niambie tu..” Kelvin alisisitiza

“Bro kiukweli ninampenda Suzana… ila siwezi kuwa na Suzana… labda abaki kuwa rafiki tu kwangu..” Jimmy alimjibu Kelvin

“kwanini Jimmy… wakati nyie mumetoka mbali sana.. mimi sitaki ninekane nimeingilia mapenzi yenu Jimmy niambie tu kama unamuhitaji Suzana…” Kelvin aliendelea kusema

“Bro mpaka sasa tayari mkononi mwako una kila kitu ambacho mwanadamu anahitaji… una pesa una nyumba nzuri una magari mazuri…. ila nasikitika .. bado hujaoa!!…” Jimmy alisema

“sasa kwanini usimfanye Suzana akawa mkewako bro…  mimi ndio kwanza nimepata nafasi ya kuja Dar kutafuta vumba.. nitampa nini Suzana sasa hivi bro..” Jimmy aliongezea

Maneno yale yalimakata maini Kelvin hakuwa na la kusema tena, alibaki kutikisa kichwa akimaanisha kuwa maneno  yale yamemuingia  vizuri.

Alimuamua kumuaga  Jimmy kuwa anaenda kulala japo bado analiwaza jambo hilo, Jimmy naye alimuambia kuwa hana muda mrefu ataenda kulala pia.

Kelvin aliingia chumbani kwake akiwa na mawazo ni wapi ataanzia kuuteka moyo wa Suzana, akilini mwake alijua kuwa historia yake si nzuri nayo inaweza kumfanya akataliwe na Suzana. Alipiga moyo konde na kujiapiza kuwa kesho angemuambia Suzana ukweli wote juu ya hisia zake.

                                   ************************************

Processing…
Success! You're on the list.

Asubuhi na mapema nilikuwa wa kwanza kuamka kabla ya wote akilini mwangu nilikuwa nawaza majina matatu tu ERIC JOHN HERMAN  mzaliwa wa Bumbuta, ukweli ni kwamba sikuwahi kumjua kaka yangu kwa sura wala kwa majina yake lakini kilichonipa wasiwasi ni majina yake ya pili JOHN HERMAN halafu amezaliwa mahali sawa nami.

Mapema niliwaamsha Jimmy na Kelvin ili wajiandae kunipeleka mahakama ambayo inaendesha kesi ya mhalifu yule.

Haikuwachukua muda sana kujiandaa, tukatoka hotelini na kupanda gari kisha tukaanza safari kuelekea mahakamani.

Tulifika pale muda muafaka kabisa muda ambao mtuhumiwa alikuwa akiletwa mahakamani kwa ajili ya kupokea hukumu yake, ni mimi na Jimmy ndo tuliweza kuingia mahakamani, Kelvin alibaki ndani ya gari.

Haikuwa ngumu kwa Jimmy kupata nafasi ya kuongea na maafisa wa jeshi la polisi ambao ndio walikuwa wanasimamia kesi ile, aliniombea nafasi ya kuongea na mtuhumiwa kabla ya kuingia mahakamani kwa ajili ya hukumu.

Kama bahati tu kwani huwa hairuhusiwi kufanya hivyo, nilipata kwenda katika chumba ambacho mtuhumiwa alikuwa amewekwa  kabla ya kupata ruhusa ya kuingia mahakamani.

Baada ya  kuufungua mlango wa chumba kile Jimmy akiwa pembeni yangu sikuweza kuamini kile nilichokisikia masikioni mwangu…

Nilimsikia Mr Herman akilitamka jina langu SUZANAAA…!! moyo wangu ulienda kasi sana nilitamani kuiambia akili yangu kuwa siyo Suzana mimi aliyekuwa akiitwa.

Mwili wangu ulihisi baridi ghafla pale aliponiita kwa mara ya pili tena Suzana John Herman, safari hii aliniita kwa majina yote matatu, kisha nilimuona akifungua mikono yake.

Akanionyesha kisanduku ambacho alikuwa amekishika mkononi mwake, nilipokiona kisanduku kile nilihisi kama umeme unapita ndani ya mwili wangu, niliyumba kidogo namshukuru Jimmy ambaye aliwahi kunidaka kabla sijafika chini.

Nilijitahidi kupiga hatua chache mbele na kumwangalia zaidi machoni pa watu alionekana kama bindamu katili, tena muuaji, kwa muda ule mbele yangu nilimuona kama kaka yangu haijalishi kuwa  ndiye ambaye aliniteka na kunisababishia maumivu yote yale.

Sikujua nini cha kufanya wakati ule nilipomuangalia zaidi nilimuona akifungua kisanduku kila kisha akatoa barua mbili zilizokunjwa na badae akatoa picha nnena kunionesha mbili zilikuwa za wazazi wetu baba na mama na zilizobaki zilikuwa ni sura yangu  na yake.

Sikuamini nilichokiona mahali pale nilihisi kama sinema tu inachezwa, nililia kwa uchungu sana, kaka yangu alitoa barua ambayo aliiandika yeye mwenyewe kwa mkono wake kisha  akaichanganya na barua zilizoandikwa na marehemu mama yetu  kisha akazifunga vizuri kwenye kisanduku kile na kunikabidhi tena.

“Suzana mdogo wangu kwa kitendo nilichokifanya sistahili hata kukuomba msamaha lakini najua unatamani kujua mambo mengi sana kuhusu mimi, muda hautoshi hapa ila natumai utaisoma barua niliyokuandikia kwaheri dada yangu Nakupenda sana”.. Eric Herman alisema

Muda wa kuongea na kaka yangu tayari ulikuwa umeisha hivyo nilitolewa nje na polisi sikutaka hata kusikiliza maamuzi ya kesi hile nilipitiliza moja kwa moja nje na kumuomba Jimmy turudi nyumbani nikapumzike.

Tulifika kwenye gari tukamkuta Kelvin akiwa anatusubiri, kwa hali ambayo aliniona nayo wala hata hakuuliza swali aliwasha gari na tukaondoka kurudi hotelini.

Watu husema kuwa “siku njema huonekana asubuhi”  tayari siku hile kwangu haikuwa njema hata kidogo tulipofika hotelini Kelvin alitueleza kuwa tusingeendelea kukaa hotelini muda wote hivyo alituomba tuende nyumbani kwake tukakae huko na kupanga mipango mipya.

Muda wote huo Kelvin alikuwa karibu nbami kuhakikisha kuwa nakuwa na furaha na kusahau yale yote yaliyonikuta, alijaribu kunichekesha na kunipa hadithi ambazo aliamini kuwa zingenifanya nijisikie vizuri.

Tulisafiri kwa gari mpaka kufika maeneno ya Sinza mahali ambako ndiko nyumba ya Kelvin ilikuwepo, tulifika pale, hakika Kelvin alibarikiwa akili ya kujenga majengo makubwa na mazuri, pesa aliyoipata hakuitumia vibaya kama wengine walivyofanya.

Sasa tayari nilishamjua kaka yangu, hila sikuwa namjua baba yangu bado japo niliwaza kuwa kile kilichoandikwa kwenye barua niliyoipata kutoka kwa kaka yangu lazima ingekuwa na maelezo kuhusu baba yangu.

Niliketi chumbani kwangu huku moyo wangu ukiwa unawaza mashujaa wawili walioko mbele yangu, yupi nimkubalie endapo wote wakionekana kunihitaji kimapenzi, wote wameyasaidia maisha yangu na bado wanazidi kunisaidia, sikupata jibu.

                                      *******************************************

Wiki mbili zilishapita tangu mambo yote yatokee, wote tulikuwa tukiishi nyumbani kwa Kelvin, siku moja nikiwa nimelala chumbani mwangu ghafla mlango wangu wa chumbani uligongwa nilipofungua mbele yangu alisimama Jimmy

“aah Jimmy kulikoni babaa…” Niliuliza kwa mshangao

“nimekuja kukuhaga Suzana… naendelea na safari yangu kama nilivyokuwa nimepanga…” Jimmy alinambia

“Unamaanisha nini Jimmy kwa kusema hivyo..” Niliuliza kwa hamaki kidogo

“Suzana siwezi kukaa hapa  muda wote nami naenda kutafuta ridhiki yangu!!..”

Sasa nilitambua kuwa Jimmy anaondoka sikuwa na uwezo wa kumzuia,

“Suzana nna jambo napenda kukuambia…” Jimmy alisema

Moyo wangu ulipiga pah! Tayari nilishajua kuwa ananipenda hivyo moja kwa moja nikafikiri anataka aanze kutupa maneno yake.

“Suzana, ni kweli nakupenda na najua unatambua ilo,  ilaa… Suzana mwanamke ni kama ua, muda wote linahitaji maji ili kuweza kuchanua.. Suzana uishi salama siku zote” Jimmy alimalizia

Alinibusu shavuni kisha akageuka na kuanza safari yake, nilimjua Jimmy ni mtu wa mafumbo sana ila fumbo hili nililivumbua kwa uelewa wangu. Nilijua Jimmy anahitaji kutafuta pesa na sio wanawake kwa wakati ule hivyo hata kama ananipenda bado anajaribu kuuzuia moyo wake kufunguka mbele yangu.

Nilimsindikiza Jimmy kwa macho hali sikujua kuwa Kelvin amebanza pembeni akiniangalia mpaka pale nilioporudisha macho akili yangu mahali nilipokuwa.

Pembeni yangu nilimuona amesimama kifua wazi, sikuwa na la kufanya macho nilitamani kuyaficha lakini moyo ulikataa, nilibaki nikimuangalia Kelvin ambaye sasa nilimuona akisogea karibu zangu zaidi.

Nilikosa cha kusema nilipatwa na kigugumizi,

“Kelvin.. Jimmy ame.oond…oka.. ataruidiii ten..a au?” Niliongea kuwa kuhema.

“Suzana tafadhali naomba unipe nafasi moyoni mwako…. naomba  uwe…. uwe…” Kelvin alibu tofauti kabisa na swali nililomuuliza.

“Kelvin… itakuw… je tafadha… Kelvin siwe….”

Kabla sijamaliza kusema neno lolote alinikumbatia na kunibusu mdomoni, alikatiza maneno yangu nami nilishindwa kuendelea ni kweli nilikuwa nampenda Kelvin lakini nisingeliweza kumkubalia kirahisi lazima nioneshe ukakasi kama mwanamke halisi.

Niliogopa Kelvin asije kuniona mwanamke wa maji mara moja, alinibusu tena mara  ya  pili kisha akanibusu tena ubaridi wa midomo yake ulisisimua mwili wangu nilijihisi nipo katika kisiwa cha mahaba, na mimi ndiyo malkia wa kisiwa hiko.

Aliniachia nafasi ya kuhema vizuri kisha akaniuliza Suzana.. naomba uniruhusu nikuoe tafadhali… nimechoka kuwa bachela..”

“Kelvin hilo siyo la kuniomba tena, tayari umeshalipata niwewe tu… lakini wacha tumalizie jambo moja kwanza…”

Niliiingia chumbani na kuchukua kisanduku kwa mara ya kwanza nilikifungua kwani niliamini tayari nimeshapata  nguvu na sababu za kukifungua, nilikisoma chote niliyoyaona sikuamini macho yangu…. baba  na mama tayari walishafariki.

Barua ilieleza kuwa mama yangu aliishi maisha ya upweke kwani baba yangu alikuwa ni mtu wa kupenda wanawake, baba yangu alifariki punde tu baada ya mimi kuzaliwa, kaka yangu hakuwa na uelekeo wowote.

Na hapo ndipo alipoamua kujiingiza katika magenge mabaya ili apate pesa ya kutulisha nyumbani, lakini nayeye alitekwa na hanasa za dunia kisha akatokomea mazima.

Nilifurahi kuujua ukweli wa familia yangu, lakini niliumia sana kwani ukweli wote haukua hata na chembe moja ya faraja kwangu bali ni maumivu tu.

Nilimkumbatia Kelvin na kumuambia “Kelvin nakupa wangu mtima naomba uulinde daima, katu usije utupa mibani nikapata tabu maishani”

Kelvin alliingiza mkono mfukoni kisha akatoa pesa nzuri iliyotengenezwa kwa madini ya dhahabu sikuamini nilichokiona mambo yalikuwa yanaenda kasi sana.

Nimetoka kwenye uchungu kisha napozwa kwa maneno matamu yaliyobeba vitendo thabiti alinishika mkono wangu kisha akachagua kidole muhimu na kuivika pete ile kiganjani mwangu…

“Suzana mpaka pale kifo kitakapotutenganisha…” Kelvin aliniambia

“Kelvin mpaka pale  kifo kitakapotutenganisha….” Nilimjibu Kelvin huku machozi ya furaha yakinitoka…..

mwisho…….

Tunakushukuru kwa kuwa nasi tangu mwanzo wa hadithi yetu mpaka sasa tumeufikia mwisho na kutambua uchaguzi alioufanya Suzana juu ya maisha na mahusiano yake…

Tafadhali tunakuomba kujiunga nasi ili uwe wa kwanza kupata hadithi na habari zetu punde tu tutakapozichapisha

KARIBU KUSOMA HADITHI ZINGINE

Penzi la wakala wa Giza; Ep 01

Penzi la wakala wa Giza; Ep 02.

Penzi la wakala wa Giza: Ep 03