SEHEMU YA NNE

Ilipoishia…

Hatua chache mbele tulisikia milio mingi ya risasi, nilipogeuka nyuma niliona miili ya wale wazee na wenzetu ambao walikuwa na zaidi ya miaka 46 na kuendelea ikiwa imelala chini inavuja damu,”wameuawa…..!!!” nilijiuliza mwenyewe nafsini mwangu, mwili wangu ulitetemeka nikajua huku tuendako hakuna usalama tena...

Nyuma yetu tuliacha miili ya wenzetu ikiwa inavuja damu, mbele yetu walikuwapo watekaji wakituongoza njia kuelekea ndani zaidi ya msitu, wenye miti mirefu na sauti za wanyama wakali, kila upande niliogeuka walikuwapo watekaji, sasa walikuwa kama kumi na tano hivi kwa ajili ya kutudhibiti.

Safari isiyo na tumaini la kufika ilianzia pale, ndoto zangu za kurudi jijini Dar tayari zilianza kupotea taratibu, nilimfikiria Jimmy, kaka niliyekutana naye kwa mara ya kwanza ndani ya basi akiwa na ndoto za kufika Dar na kutimiza malengo yake…. nilijuwa kabisa ndoto zake zinapotea..

Tulitembea mwendo wa dakika kumi kisha tukatokeza kwenye barabara, kati yetu hakuna ambaye aliweza kutambua pale ni mahali gani kila mmoja wetu akili alielekeza moyo wake katika maombi na ibada ya kimya kimya akiomba Mungu aweze kutoka kwenye mkasa huo.

Ndani ya moyo wangu muda mwingine nilihisi kama ni ndoto hivi, lakini kila nilipopiga hatua kukanyaga ardhi na kusikia maumivu chini ya nyayo zangu hapo nilitambua dhahiri kuwa sipo ndotoni.

Tulisimama kando ya barabara, punde likaja Lori likiwa tupu na sisi sote tuliamrishwa kuingia ndani ya lori hilo na hapo tayari ilishatimu saa saba kamili, nilimuona Jimmy akipambana aje akae mahali ambapo nilikuwa nimekaa hapo nilitambua kuwa Jimmy ananithamini sana hata kama  ndio kwanza tumekutana.

Baada ya kujipanga ndani ya lori lile walikuja watekaji watatu wakiwa wamebeba vitambaa vyeusi na wakaanza kutufunga vitambaa vile usoni ili tusiweze kuona wapi tunakwenda.

Mikono yetu yetu ilifungwa kwa nyuma, macho yetu yalifungwa vitambaa na hatukuweza kujua wapi  tulikuwa tukipelekwa, wakati huo nilimsogelea zaidi Jimmy na kukaa karibu naye.

Safari ilianza kama vile watuhumiwa na polisi ndani ya difenda, wote walikuwa kimya na watekaji wetu nao walikuwa bize na mambo yao kwani tayari walijua wameshatuweza na hakuna mwenye ujanja wa kuweza kutoroka.

Ndani ya lori ni moshi wa bangi tu ndio ulitapakaa, bangi zilizokuwa zikivutwa na watekaji wale. Niligusa kiunoni pangu mahali ambapo nilikuwa nimetunza kile kisanduku cha mama yangu, nilijiridhisha kuwa kipo salama…

“Suzana Herman… nafurahi kukufahamu.. japo katika wakati mgumu!!” Jimmy alininong’oneza.

“Jimmy nafurahi pia kukujua… Jimmy wewe ni kijana mzuri sana…” nilimjibu taratibu sana.

“Suzana kwa lolote litakalotokea nakuahidi nitakulinda… uwe salama wakati wote..” Jimmy aliniambia..

“Jimmy haina haja ya kusema yote hayo… mimi sina cha kupoteza hapa duniani, niko mimi tu hata niki…” Jimmy alinikatisha kabla sijamaliza..

“Suzana huwezi kufa mahali hapa..  endapo mimi nitakuwa hai.. huwezi Suzana..” Jimmy aliniambia.

“Suzana… kama endapo maisha yangu yataisha leo… jua tu kuwa nimekupenda..  tangu mara ya kwanza ulipoonesha tabasamu lako kwangu…” Jimmy alisema

“Jimmy usiseme hivyo tafadhaliiii… bado tuna maisha mengine ya kuishi Jimmy…” nilimuambia Jimmy huku nikihisi maji ya moto moto yanachuruzika mashavuni mwangu… machozi!!..

“Suzana tangu nilipohisi kuumia kwa ajili yako… tangu nilipotamani nikutetee kwa namna yoyote… tangu nilipokuona kwa mara ya kwanza… moyo wangu uliachia kwako.. nisingeweza kusema mapema hivii…” Jimmy alininong’oneza sikioni pangu taratibu..

“Sina budi kuweka wazi kile ninachohisi moyoni mwanangu Suzana… mapenzi ni kama maua mazuri mlimani, nyakati zote huchanua…  huenda hii ikawa pumzi yangu ya mwisho kwangu… nitafurahi na kujiita shujaa nikifa huku natetea uhai wako Suzana…. nitapambana utoke mahali hapa ukiwa hai..” Jimmy alisema maneno yale kwa uchungu sana…

Moyo wangu ulihisi uchungu sana, maneno yake Jimmy yaliuchoma moyo wangu barabara ni kweli alikuwa ameongea maneno ya uchungu kiasi cha kugusa dunia iliyobeba hisia za mapenzi tangu ya moyo wangu.

Kabla sijajibu kitu chochote kwa Jimmy nilihisi mkono ukigusa uso wangu, sikuweza kujua ni nani amenigusa nilianza kuhisi labda angekuwa Jimmy ndo ameamua kujitoa muhanga kwa ajili yangu..

Ghafla niliona mkono ule ukifuta machozi yaliyokuwa yakinibubujika kutokana na maneno ya uchungu niliyoyasikia kutoka kwa Jimmy, baada ya kunifuta machozi taratibu alikitoa kitambaa cheusi kilichokuwa kimeziba macho yangu.

Kufumba na kufumbua sura ya Black heart mbele ya uso wangu…!! moyo wangu ulienda mbio ghafla uoga ukanijaa, nikahisi kifo tayari kipo mbele yangu.. Kabla sijasema neno kaka yule alisogea karibu nami kisha akanieleza kuwa.. “usihuzunike mrembo, kila jambo unaweza kuchagua kusuka au kunyoa” kisha akanifunga tena kitambaa usoni maneno yake

yalinifanya kuhisi kama huko tuendako wanawake hubakwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili wakidanganywa kusamehewa, nilichukia sana maneno yake moyo wangu uliumia sana.. 

Baada ya kwenda mwendo wa gari kwa nusu saa ghafla gari lilisimamishwa na wote tukatolewa vitambaa usoni na kufunguliwa minyororo iliyokuwa imefunga miguu na mikono yetu kisha tukaamriswa kushuka kutoka kwenye lile Lori..

Mbele yangu niliiona Ngome iliyojengwa kwa miti na nyasi tupu kama vile kambi za wanajeshi wa kivietinami, hapo nikajuwa kuwa tayari tumeshafika mwisho wa safari, wote tukaamrishwa kuingia ndani kwa mstari kama ilivyo ada kwani tayari tulishakuwa watumwa wao.

Tukiwa getini kabla ya kuingia ndani kabisa, yule baba ambaye tulipanda naye kutoka hotelini alituambia kuwa tutapitia katika vyumba viwili kwa ajili ya ukaguzi, wa mwili mzima ili kuhakikisha hatuingii ndani ya ngome yao tukiwa  tumebeba kitu chochote kutoka nje.

Moyo wangu ulikuwa unadunda mno kwani nilijua kuwa kiunoni kwangu nimefunga kisanduku kidogo anbacho nilipewa na mama yangu, nami sikutaka kukipoteza hata mara moja.

Nilisimama kwenye mstari nikiwa nawaza itakuwaje nikingiia ndani mule kwenye ukaguzi?… nilipiga moyo konde, nikasali kwa Mungu wangu kisha nikakaa kitako kusubiri zamu yangu.

“kila jambo huwa mwisho” hivyo ndivyo ilivyokuwa pale nilipomuona Jimmy akipiga hatua kadhaa mbele akiingia kwenye chumba cha ukaguzi, nami nikabaki nje kusubiri zamu yake ilipita nami nikafuata lakini hapo sikuweza kumuona Jimmy kwani tayari alishatolewa na kupelekwa chumba kingine.

Niliingia kishujaa moyoni mwangu niliamini kuwa tayari Mungu niliyemtegemea ameshatia wepesi katika jambo ambalo lilikuwa mbele yangu, niliufungua mlango wa kuingilia chumba cha ukaguzi, kisha nikaingia ndani.

“Looh!! Sura niliyoiona ilinishtua sana..”  sura ya kijana mweusi tiii..!, amekomaa, amesimama kama mwanajeshi wa anga ooh!!, alikuwa yule mkaka waliyemuita Black heart moyo wangu ulipiga sana, akilini mwangu niliwaza kuwa tungekaguliwa kulingana na jinsia zetu lakini haikuwa hivyo.

Nilisimama sehemu ambayo niliambiwa kusimama, akanifuata.. akasogea zaidi karibu yangu.. akaniangalia kwa makini kisha akaniuliza.

“unaitwa nani mrembo…?” Black heart akiniuliza..

Mwili wangu ulisisimka, uzito wa sauti yake uliongeza mapigo ya moyo wangu,  kwani nilijuwan baada ya jina kilichofuata ni kuambiwa kuvua nguo zangu.. machozi yalianza kunitoka kabla ya kujibu swali.

“unaitwa nani mrembo?… usinifanye nirudie tena”. Black heart alinisogelea zaidi na kuniuliza kwa mara ya pili.

“Na..itwa Suzzie.. Suzana Herman..!!..” nilijibu huku machozi yakinitoka.

“Sawa Suzana…najua unaelewa umeingia katika chumba hiki kufanya nini…. vua nguo zote..” Black heart aliniambia

“Tafadhali kaka yangu nakuomba… tafadh…” Niliamuangukia miguuni na kumpigia magoti huku nikimwomba Mungu anisaidie kulegeza moyo wa kaka yule..

“Nimesema vua nguo… mimi sio mama yako mpaka unililie hapa…” Black heart aliniambia

Hapo sasa alikuwa amegusa chemba nne za moyo wangu, alipotaja mama yangu, moyoni mwangu nilijuwa kuwa mama yangu alifariki dunia kwa kifo cha uchungu na maumivu sana.

Kilio changu kiliongezeka maradufu, kilio cha kwikwi nilimuangalia  kwa uchungu huku nikiwa nimempigia magoti alinishika mabegani mwangu na kuniambia nisimame, amri yake bado ilibaki palepale kuwa lazima nivue nguo.

“uso wa mwanadamu umeumbwa na aibu” moyoni mwangu niliamini hili siku zote, akili zilinijia tukiwa wawili tu chumbani mule, niliwaza kuvua nguo zangu nitaonekana mwili wangu na mwanaume ambaye sio mume wala mpenzi wangu, pia nilijuwa kuwa kufanya vile lazima kisanduku changu cha siri kingeonekana  hivyo nilitakiwa kutumia akili ya ziada.

Nilianza kuvua nguo yangu ya juu taratibu huku nikiwa nimekaza macho yangu kwake, sijui ujasiri hule niliutoa wapi wakati siku zote huwa siwezagi kumuangalia mwanaume usoni namna ile.

Nilimtazama barabara huku natoa nguo yangu ya juu, tayari sasa nilikuwa nimeshaishusha kiasi cha matiti yangu kuanza  kuonekana, nilimuona kaka yule akirudi nyuma hatua moja, na kutazama chini hapo ndipo nilipothibitisha kuwa ni kweli uso umeumbwa na aibu.

Nilipogungua kuwa nimeanza kushinda ule mchezo niliamua kupigilia msumari mwingine hapohapo

“nivue zaidi ya hapa” kwa sauti ya upole iliyojawa na mahaba ya chumbani nilimuuliza, niliamini kuwa kumbinyia sauti kungemfanya arudishe hisia za kibinadamu kwani wakati ule alikuwa kama simba mbele ya swala.

Jitihada zangu zilizua matunda aliponishika begani na kuniambia basi inatosha nitakukagua hivyohivyo, haraka nilirudisha nguo yangu ya juu sawia  sikuweza kujali kama aliyaona matiti yangu ila nilichoshukuru ni kwamba sikuvua nguo zangu zote.

Sasa alianza kunipapasa kuanzia miguuni kama vile wapelelezi wafanyavyo pale wanapomuhisi mtu kuwa ana silaha au kitu chochote cha hatari, alinipapasa mpaka akafikia kiunoni pangu hapo tayari nilijuwa kisanduku changu lazima kijulikane tu sikuwa na la kufanya.

Haikuwa bahati kwangu saa hiyo alihisi uvimbe kiunoni kwangu na kuniuliza..

“umeficha nini Suzana… nini hiki?” aliniuliza

Nilijaribu kudanganya lakini alikataa katakata na kuniamrisha nikitoe, basi sikuwa na budi nilitoa kisanduku changu mbele yake na kumuonesha.

Alikichukua na kunambia niende nje nikajiunge na watu wengine ukaguzi wangu umeishia hapo, nilishindwa hata kupiga hatua mpja nikiamini kuwa tayari nimeshapoteza tena siri na majibu ya maswali yangu kuhusu familia yangu.

Niliwaza ni wapi ningempata kaka yangu endapo ningepoteza kisanduku kile au ni wapi ningeweza kumpata baba yangu endapo ningepoteza kisanduku kile, niliumia sana.

Kama bahati tu kaka yule alinambia kuwa “nitakitunza kikasha chako, lakini hutakiwi kumuambia mtu yeyote na nitakupatia baada ya kuona hakina madhara yoyote kwetu…” nilimshukuru hata kwa lile nililosikia kutoka kinywani mwake.

Nikaamua kutoka katika chumba cha mahojiano na kujiunga na watu wengine ambao tayari walikuwa wameshakaguliwa…

Baada ya muda mchache watu wote tulishakaguliwa tayari, tuliongozwa kuelekea kwenye chumba kikubwa mno ambacho kilikuwa kimejengwa kwa miti na kuezekwa nyasi tuliambiwa mkuwa hapo ndipo mahali ambapo tungelala.

Sikuweza kujua ni saa ngapi kwani sikuwa na saa yangu vyote nilinyang’anywa, japo kwa makadirio yangu nilitambua tu kuwa ingekuwa zaidi ya saa nane usiku.

Bila vitanda wala mashuka ya kujifunika,  bila makoti baridi ilitupiga usiku kucha bila uwoga wala aibu nilijibanza ubavuni mwa Jimmy… alinikumbatia na kunipa faraja usiku ule.

Sikuweza kupata hata lepe la usingizi, hakuna aliyeweza kulala usiku ule zaidi ya watoto wadogo ambao nao walichukuliwa pamoja nasi Jimmy alikuwa shujaa wangu usiku ule, aliujaza moyo wangu kwa maneno matamu, maneno ya kunipa faraja na nguvu ya kutoogopa hata kama nipo hatarini.

                             *****************************

“Suzana mwanangu mpendwa,

Ukiona ujumbe huu ujue mama yake siko hai duniani, mwanangu kwenye tumbo langu alizaliwa kaka yako kabla ya kuzaliwa wewe, maisha yetu hayakuwa mazuri, nilimlea kaka yako katika tabu na majonzi tele yalliyosababishwa na uchafu wa baba yako.

Mapenzi kwa wanawake wengi, ndoa za mitala unywaji wa  pombe uliopitiliza hizo ndizo zilikuwa tabia zilizokubuhu moyoni mwa baba yako nilimvumilia lakini nilishindwa mwezi mmoja baada ya kuzaliwa kwako.

Baada ya miaka miwili baada ya kutengana na baba yako, nilisikia amefariki dunia kwa ugonjwa wa ukimwi nilihuzunika moyoni na nikajiapiza kutohitaji kumkumbuka tena milele, kaka yako aliondoka ukiwa mdogo sana alisema anaenda kutafuta maisha.

Nilimtakia baraka tele ila kila siku ziliposonga taratiba haiba yake ikaanza kupotea na kurudi kwake nyumbani kukawa ni ndoto, mwanangu tafuta pesa za kutosha uweze kuwa na maisha ya mazuri fanya kila kilicho chema na halali, Mungu atakujalia mara dufu

NAKUPENDA SUZANA”

Hisia zilizojawa na uchungu zilimjaa kijana yule, alijuta kwanini alifungua kisanduku kile ambacho hakikumuhusu, maneno yenye huzuni ambayo yalikuwa yameandikwa kwenye kile kisanduku cha Suzana yalirudisha nyuma kumbukumbu zake.

Alikumbuka miaka alipokuwa mtoto mama yake na baba yake walivyokuwa wakipigana, aliumia sana… alikumbuka baada ya baba yake kusafiri nchi za mbali akiaga kuwa ameenda kutafiuta maisha na hakurudi tena miaka 15 sasa.

Alikumbuka hata siku ya kwanza anamuaga mama yake kuwa anaenda kutafuta maisha jijini Dar es salaam, na hatimaye akaishia katika utekaji watu.

Aliikumbuka siku ya kwanza alipokutana na rafiki yake Faraji ambaye alimshawishi hata akaingia katika genge la uuzaji wa madawa ya kulevya ili wapate pesa na kumtumia mama kijijini yake ambaye kwa wakati huo alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya UTI.

Akiwa peke yake juu ya mti machozi yakiwa yanamtoka moyoni wake alijisemea kuwa, “nimeuza madawa ya ulevya, nimeibia watu wasio na hatia, nimeua na sasa nauza watu nchi za mbali ili nipate   pesa” aah!! Natamani kuacha kazi hii…

Tayari roho ya ubinadamu ilianza kumuingia Black heart, moyo wake uliuma sana kwa kukumbuka mambo ambayo alikuwa akiyafanya huko awali, alipofungua barua ya pili alikuta maandishi makubwa yaliyosomeka kuwa “SUZANA MWANANGU HAIJALISHI MWANZO WETU ULIKUWA MBAYA KIASI GANI, KUMBUKA HISTORIA HAIWEZI KUBADILISHA WAKATI UJAO… ILA WAKATI ULIOPO SASA, FANYA KAZI YA HALALI KWA BIDII MUNGU ATAKUJALIA, MWISHO KABISA MTAFUTE KAKA YAKO MUISHI PAMOJA, NI MIMI MAMA YAKO BI SAUDA.

Maneno yale yalimpa fundisho Black heart, jambazi aliyeaminiwa katika kazi ya utekaji wa watu na kuwauza nchi za mbali alirudia tena kusoma maneno yale, akajiapiza ndani ya moyo wake kuwa ataacha kazi ya ujambazi na utekaji watu.

Alirudisha kila kitu ndani ya kile kisanduku bila kujua kuwa ndani ya kisanduku kile kulikuwa na vitu vingine zaidi ambavyo hakuviona alilifunga sanduku lile kisha akashuka mtini na kuelekea chumba ambacho alikuwamo rafiki yake waliyemuita Faraji ambaye alijulikana kama Jemedari katika jina lake la kazi.

Aliingia ndani alimkuta Faraji akiwa penzini na mwanamke mmoja ambaye naye pia ni jambazi kama wao, wawili hao walianza mahusiano ya mapenzi kwa muda mrefu takribani miaka miwili,  alimuomba Faraji atoke nje wazungumze mara moja Faraji hakusita alimuacha mwanamke wake kisha akatoka nje.

“Faraji tazama usiku ulivyo na kiza kinene… nasi tulikuwa mashujaa wa uovu kila kiza kilipotanda…” Black heart alisema kwa majuto.

“wingu zito limetanda moyoni mwangu…  sijui lipi jema lipi baya mbele yangu..!! “

“Black…. una nini damu yangu..?” Faraji aliuliza..

Black heart alianza kueleza juu ya mpango wake wa kutaka kuacha kazi ya ujambazi na kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine, alimueleza pia juu ya azimio lake la kutaka kumkomboa mateka mmoja na kuondoka naye…

Kabla Faraji hajajibu kitu redio kolu zao ziliita na kuwajulisha kuwa zamu yao ya kwenda kulinda mateka imewadia, hivyo walitakiwa kuchukua silaha zao na kwenda lindoni.

Faraji aliingia ndani haraka na kumuaga mpenzi wake kuwa muda wake wa lindo umeshawadia hivyo anaenda lindoni na hatorudi mpaka asubuhi.

Black na Faraji walichukua silaha zao kisha wakaelekea sehemu ya lindo, kule walikuwako watu wengine wawili ambao walisaidiana nao katika lindo mmoja wapo alikuwa akiitwa Juba ambaye ndiye alikuwa kibaraka mkubwa wa Boss wao wa kazi..

Wakiwa lindoni  Black alikumbusha tena suala la yeye kuacha kazi ya ujambazi na mpango wake wa kutorosha mateka aondoke nao.

Faraji akamwambia “ Bro huwezi ondoka na mateka itakuka kwako bro…”

“kwanini.. Jemedari wangu… nisaidie kuwazima hawa vibaraka.. mi nasepa nao hawa” Black alisisitiza

“Nisikilize kwa makini ndugu yangu… huwezi! Nimesema huwezi!.. nitakusaiudia kutoroka ila kwa sharti moja tu..”

“Unatakiwa ujue ukikamatwa tu umekufa!!…. hakuna kunitaja hata iweje..!! hakikisha hukai tena mahali pale fanya mpango uende mbali sana..! na utaondoka na mateka mmoja tu… utaweza masharti yangu?.. Faraji aliuliza

Black aliwaza kwa muda kisha akauliza “kwanini niondoke na mateka mmoja… kwanini usinipe hata watano hata kumi?”

“Nisikilize… niliagizwa na boss kuwahesabu mateka… nikarudisha jibu kuwa wako 31 jumla, sasa endapo utachukua mateka tano au zaidi, idadi itapungua sana ni heri mmoja ninaweza kutetea kuwa nilikosea kwenye mahesabu bro” Faraji alieleza.

Black heart hakuwa na budi kukubaliana na jibu alilopata kutoka kwa Faraji aliwaza ni nani angemkomboa alipata jibu la haraka kisha akarudi tena kwa Faraji na kumwambia amsaidie katika ukombozi wake.

Faraji alimkubalia kumkomboa mateka yule ambaye Black alimchagua, bila mtu yeyote kujua njama zao walipanga mbinu jinsi ya kumkomboa mateka huyo mpaka jinsi Black atakavyotoroka naye na sehemu ya kufikia.

Saa kumi alifajiri zoezi la kutorosha mateka lilianza, lilishapangwa kudumu kwa muda wa nusu saa tu… kama walivyokubaliana Faraja alijidai kuwaita walinzi wengine ambapo walikuwa lindo pamoja nao usiku ule.

Baada ya zoezi ila kukamilika na kujiridhisha kuwa hakuna mtu mwingine yeyote ambaye anaweza kuwaona Black alichomoka fasta na kuingia chumba walichowekwa mateka.

Alifika mpaka mahali ambapo Suzana alikuwapo, alimkuta amelala kwa unyonge kifuani pa Jimmy alimuamsha na kumwambia kuwa anamuomba nje, Suzana hakupinga kwani alijua kuwa yule ndiye kijana ambaye alichukua kisanduku chake.

Black alimchukua Suzana na kumpitisha kwa siri mpaka chumba kingine kilichojengwa kwa makuta ya mnazi kisha akamuuliza

“yule mkaka una eje ni mumeo au..”.

“hapana tumekutana tu kwenye gari…” Suzana  alijibu

“Sawa nina mpango nataka nikutoe mahali hapa… nataka nikutoroshe uende mbali sanaa..”

“Sawa lakini ukifanya hivyo naomba umtoroshe na yule kaka… sio peke yangu ..” Suzana alijibu

Black aliwaza kwa muda alijua ni jambob ambalo haliwezekani, alichukua dakika tano  kumweleza Suzana juu ya mpango wake…

“Kwanini unataka kunitorosha na kusaliti wenzako?..” Suzana aliuliza

“Suzana hilo sio jambo la kujua sasa hivi… hatuna muda “

Black alimuambia Suzana abaki katika chumba kile na asitoke, Suzana alikubali kutii amri hiyo.

Black alitoka haraka na akarudi katika kile chumba cha mateka alienda moja kwa moja mpaka mahali ambapo Jimmy alikuwa amekaa alifika kisha akamuambia jambo am balo alikuwa ameazimia kulifanya kwa Suzana.

Jimmy hakupinga kwa lolote ila alimhusia Black kuwa asije kufanya uzembe utakaogharimu maisha ya binti yule kwani tayari alishaanza kumpenda.

Pia Jimmy alimuomba Bla ck kuwa kama inawezekana aende kumuona Suzana kwa mara ya mwisho ili hata amuage, lakini Black bado alisisitiza kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yao mwenyewe kwani wakikamatwa adhabu yao ni kifo cha hadharani.

Black alitoka chumbani mule akimwacha Jimmy analia kwa uchungu, alipofika nje alitoa ishara kwa Faraji bila walinzi wengine kugundua kisha akaondoka kuelekea mahali alikomwacha Suzana.

Tayari dakika kumi zilikuwa zimeshakatika, alipofika alimkuta Suzana akiwa amejiinamia chini analia Black aliona kuwa ule sio muda wa kuulizana unalia nini alimuinua juu kisha akamuuliza..

“umewahi kushika silaha tangu uzaliwe..?”

“Hapana sijawahi…” Suzana alijibu

Black aliushika mkono wa Suzana kisha akatoa kisanduku na kumpatia, akamwambia kuwa natumaini sasa nitakuwa nimetimiza ahadi yangu kwako, naomba uamini kuwa sasa nimeazimia kukuokoa dhidi vita hii iliyo mbele yako..

Suzana alikiangalia kisanduku kila huku machozi yakimtoka moyoni mwake alimshukuru Black kwani hakuamini kuwa angekipata tena kisanduku kile alijikuta akimkumbatia bila hata kujua..

Black alimshika mkono Suzana kisha akamuambia tukimbie hatuna muda wa kupoteza hapa, walianza safari yao kutoroka katika ngome ya watekaji, Black ambaye naye ni mtekaji wa kuaminika aliazimia kweli kweli kuacha kazi yake hata akamtorosha mateka nna kukimbia naye.

Zoezi lao la kukwepa walinzi liliwachukua kama dakika tano hivi hatimaye walifanikiwa na kutokomea katika giza nene… walikimbia bila kugeuka nyuma Suzana alionekana kuchoka mno.

“Black tafadha…li.. siwe..zi kuendele..a …ten..a nimechoka!!..” Suzana alisema huku akihema.

Black alimuangalia akajua ni kweli amechoka, taratibu aliiinama na kumuambia panda mgongoni twende, Suzana alikataa kupanda mgongoni alimuambia kuwa anahitaji kupumzika na kama atamucha basi amuache tu yeye haendi mbele tena.

Black alimuangalia Suzana kwa huruma alimuinua kwa nguvu kisha akambeba begani, kama vile mwanajeshi vitani anapombeba mwenzie aliyepata majeraha… hakika Black alikuwa ameiva katika kazi yake.

Suzana hakuujua ni kivipi alinyanyuliwa na  kujikuta begani mwa Black safari yao iliendelea bila kukoma, hatimaye walifika mahali ambapo ndipo black alielezwa na Faraji kuwa panaweza kuwa mahali salama kwa kupumzika.

Kilikuwa ni kijibanda kidogo tu ambacho kilijengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi waliingia ndani ya kibanda hicho.

Tayari dakika ishirini na tano zilikuwa zimeshakwenda, Black alimuangalia Suzana kwa huruma kisha akamuambia kuwa anahitaji kurudi katika ngome kuhakikisha kila kitu kipo sawa na hakuna anayegundua kuwa yeye ametoroka.

Suzana alimshika mkono Black na kumuomba asiondoke na kumuacha peke yake anaogopa anahisi anaweza kuvamiwa na watu wabaya.

Lakini Black alimtoa hofu Suzana akamkabidhi bastola na kumuelekeza jinsi ya kujihami endapo kitu chochote kibaya kinaweza kutokea kisha akamuaga na kumwambia amsubiri kwani lazima atamrudia tena.

Suzana alimuangalia Black usoni kisha akamshukuru sana mpaka pale alipomfikisha, aliachana kipande cha nguo yake na kumkabidhi mkononi kisha akamuambia akipeleke kwa Jimmy ikiwa kama ni sehemu ya asante kwake… hakuwa na kitu chochote cha thamani cha kumpa kulipa fadhila zake.

Black bila kuchelewa alitoka mbio kurudi katika ngome tena, alijua kuwa amechelewa sana hivyo hakuwa na muda wa kupumzika njiani.

Hatimaye alifika tena ndani ya ngome kwa njia zake za panya alijitahidi asionekane na mtu yeyote yule.. alitembea kwa kujificha ficha hadi akaenda kuibukia katika chumba cha rafiki yake Faraji.

Aliangalia saa yake ya mkononi tayari ilishatimu saa kumi na moja alfajiri, alibadilisha buti zake kwani zilikuwa zimeshika udongo wenye rangi tofauti na pale ngomeni.

Baada ya kujiweka sawa alirudi lindoni kisha akakutana na Faraji bila mtu yeyote kufahamu nini kilikuwa kikiendelea usiku ule hali ilionekana shwari tu.

                                 *******************************************

Asubuhi na mapema mlio wa helikopta ulisikika msituni pale,  tayari siku mpya ya kazi ilishawadia kila mmoja alikaa chonjo kumpokea mgeni aliyekuja kwa helikopta.

Ilitua ndani ya ngome, baada ya mazingira kuwa shwari alishuka m’baba mmoja aliyejulikana kwa jina la Mr. Escobar ambaye kwa haraka haraka alionekana ni mwenye asili ya Mexico.

Nywele zake za kizungu zilimpa muonekano mzuri, alishuka taratibu kwenye helikopta akiwa anaongozana na wapambe wake wanne, watatu wenye asili ya kizungu na mmoja ni Mtanzania.

Walipigiwa saluti kutoka kwa Black heart na wenzake ambao ndio walihusika katika kufanya uhalifu wa utekaji wa binadamu.

Baada ya kupokea saluti hizo walielekea moja kwa moja katika chumba ambacho walikutana na kodineta wao ambaye  ndiye m’baba aliyepanda basi kutoka hotelini na hatimaye kufanikisha zoezi zima la utekaji.

Walimsalimu kisha walianza kupanga mikakati jinsi ya kusafirisha mateka wale. Mr Escobar alieleza kuwa wamekuja na magari ya mizigo ambayo wataweza kuyatumia kusafirisha mateka hao na asiwepo wa kujua.

Baada ya kuweka mambo yote sawa Mr Escobar alitoa begi na kumkabidhi yule m’baba ambaye amefanikisha zoezi zima.

“Here’s your 500 Millions Mr Herman, thanks for your  fully cooparation “ (Hizi ni pesa zako milioni 500 Mr Herman) Mr. Escobar alisema.

Mr Herman ambaye ndiye m’baba aliyepanda basi kutoka hotelini na kufanikisha zoezi zima la utekaji wa abiria alifungua begi lile na kuangalia ndani yake, alikuta noti nyingi za Kitanzania hakuwa na wasiwasi kwani kazi hiyo alikuwa ameifanya kwa muda mrefu akishirikiana na watu mbalimbali kutoka nchi za nje.

Alichukua begi lile kisha wote kwa pamoja wakatoka nje na kuelekea mahali ambako helikopta ilitua.

Baada ya dakika chache yalifika malori mawili ya kubeba  mizigo ya masafa marefu tayari kwa kupakiza mateka na kusafirisha kuelekea mpakani mwa Tanzania na Malawi ambako huko mateka wangehifadhiwa kwenye ngome ya Mr Escobar kwa siku kadhaaa na kutengenezewa uraia bandia kisha kusafirishwa kwa ndege inayomilikiwa na Mr Escobar mwenyewe,

Mr Herman alitoa amri kwa vijana wake kuwa wawalete mateka wote wakiwa wamefungwa nyuso zao, walifanya kama walivyoagizwa.

Black aliona kuwa huu ndio muda muafaka wa yeye kufikisha ujumbe alioagizwa na Suzana, aliingia chumba cha mateka haraka kabla  ya wenzake kuingia alifika moja kwa moja mahali ambapo Jimmy alikuwako.

Akampatia kitambaa kile na kumuomba akiweke mfukoni, Jimmy alikiangalia kwa umakini kisha akatambua kuwa ni kipande cha nguo iliyokuwa imevaliwa na Suzana, Jimmy alimsogelea Black na kumuuliza umemfanya nini Suzana.

Black alijitetea na kujaribu kumueleza kuwa Suzana mwenyewe ndiye ambaye alimpatia kipande kile ili aje akambidhi na iwe kama ahadi kwake kuwa atafanya jitihada zozote amsaidie katika janga lile.

Kabla Jimmy hajajibu chochote tayari walinzi wengine walishafika mahali pale hivyo hakukuwa tena na nafasi ya kuongea kati yao,  Black alimnyanyua Jimmy na kumfunika uso wake kwa kitambaa kama wengine kisha akamnong’oneza kuwa Suzana ameahidi kukukomboa hivyo usijali Jimmy.

Kwa siri tayari Black aliingiwa na roho ya ubinadamu kiasi cha kuwasaliti wenzake bila hata ya kujali matatizo yatakayowapata alitoa kisimu kidogo cha mkononi kisha akakitia mfukoni mwa suruali ya Jimmy na kumnong’oneza…

“mfukoni mwako nimeweka kisimu kidogo, kimeunganishwa vizuri na mtandao wa GPS kina laini na vocha kutosha unaweza kupiga nchi yoyote muda wowote, wewe ni mwanaume shujaa, chagua moja kuwaokoa wote hao au kujiokoa mwenyewe”

“sasa unasafirishwa kuelekea malawi, huko ulinzi utakuwa mkali wa kutumia mashine na vinasa sauti ukikamatwa na hii simu adhabu ni kifo, Jina lako la siri utaitwa Serena kila la kheri” Black alimalizia.

Machozi ya furaha na shukrani yalianza kumtoka Jimmy kwani ni kama alianza kuona hatima yake baada ya kupewa maneno ya kishujaa na Black, hakuweza kujibu neno lolote alibaki kimya tu.

Walitolewa nje mateka wote kisha wakapandishwa ndani ya malori kama mizigo, watoto walikuwa wamechokoa kwa kulia, watu wote walikuwa wamechoka kwa shuruba waliyoipata kwa muda wa siku moja tu.

Mr Escobar alifanya idadi ya mateka na kukuta wako 31  kamilifu alimshukuru sana Mr Herman kisha wakapanda helikopta yao na kuondoka, huku magari nayo yaliwasha injini na kuondoka wakipitia barabara za panya kuelekea Malawi.

Black alibaki amesimama tu asijue la kufanya , alibaki amemtazama Faraji mdomo wazi tu hukua akijiuliza imekuwaje mateka wamebaki idadi ileile 31 wakati mmoja ambaye ni Suzana alimtorosha, alijiuliza moyoni au Suzana aliamua kunifuata kwa nyuma na kurudi tena kwenye kundi la mateka kwasababu ya Jimmy?.

Alishindwa kupata majibu ya mawazo yake, alitamani kupata mgawo wa pesa yake kisha aende kuangalia mahali ambako alimuacha Suzana.

Mr Herman ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wao aliwaita chumbani idadi yao sasa walikuwa vijana tisa ambapo nayeye mwenyewe alikuwa wa kumi baada ya vijana wengine kuondoka na Mr Escobar kwa ajili ya kulinda mateka.

Aliwaambia kuwa tumepata shilingi milioni mia tano kama ambavyo niliwambia hapo awali Escobar hanaga longolongo linaokuja suala la kazi.

Kwahiyo tutagawana kama tunavyofanya siku zote nitachukua milioni mia moja taslimu kisha mia nne zinaobaki nitazigawa kwenu.

Bila kupinga kila mmoja alitoa begi lake tayari kwa ajili ya kuwekea fedha Mr Herman alitoa mashine kwa ajili ya kuhesabia pesa zao.

Waligawana pesa zao kila mmoja alichukua zaidi ya miliona 44 huku Mr Herman akichukua milioni mia moja, baada ya mgawo aliwaruhusu vijana wao wende majumbani mwao kwa ajili ya mapumziko nayeye atamalizia kazi zilizobaki ngomeni hapo.

Kila mmoja alienda sehemu ambako huwa wanapaki magari yao,  waliwasha magari yao na kuondoka Black alimkumbusha Faraji kuwa walitakiwa kupitia mahali ambako walimuacha Suzana.

Haikuwachukua muda mrefu mpaka kufika mahali ambako Black alimficha Suzana, walishangaa kutokuta dalili ya mtu mahali pale.

Black bila kufikiri alianza kutokwa na machozi akijua tayari ameshampoteza Suzana akili yake ilimtu kuwa tayari Suzana amerudi kule kwenye mateka na kujichanganya nao ili awe karibu na Jimmy.

“ndio maana mateka walitimia 31 tena… ouya Jemedar wangu huyu binti atakuwa alirudi tena kule ngomeni na kujichanganya nao… dah” Alisema Black

“Hapana Black hajarudi kule… angerudi kule basi idadi yao ingekuwa 32 na sio moja tena..” Faraji alijibu.

“Faraji ebu niambie kipi unanificha rafiki yangu…mbona sikuelewi”

Faraja alianza kumueleza jinsi alivyoucheza mchezo mzima, alimuambia kuwa mateka walikuwa 31 jumla, baada ya kumtoa Suzana wakabaki 30.

Lakini namba ilirudi 31 kwani mpenzi wake naye alijiunga na mateka baada ya Suzana kutolewa, bila mtu yeyote kufahamu hilo.

Akamueleza kuwa mpenzi wake alikuwa akitamani sana kwenda nchi za nje hivyo ile aliona kama ni nafasi nzuri kwake, usiku ule aliandaa vifaa vyake vya kuondokea ikiwemo nguo ambazo angevaa kama mateka.

“Nisikilize Black mimi nilijaribu kumshauri asifanye hivyo lakini hakunisikia tayari mawazoya kwenda nchi za nje yalishaota mizizi kichwani mwake” Faraji alisema

“hata hivyo asingeweza kkusafiri kwa njia za kihalali kwani yule ni moja kati ya wanawake tano wanaotafutwa nchini kwa makosa ya kuuza madawa ya kulevya, hivyo hata mimi niliona njia ile ni sahihi japo inaniuma sana..” Faraji aliongeza.

Black aliishiwa nguvu akabakin amekaa chini asijue la kufanya, walikaa pale kwa muda wa dakika kumi wasijue la kufanya.

Hatimaye Faraji alimwambia Black heart kuwa waondoke na kurudi nyumbani kwani huenda Suzana ameamua kujisaidia mwenyewe na kusonga mbele, waliiingia kwenye gari.

Kabla hawajawasha gari walisikia sauti ikiita majina yao, Black alikuwa wa kwanza kushuka  kwenye gari alishangaa kumuona Suzana akiwa anakimbia huku anahema mno.

Alimkimbia na kumkumbatia alimuangalia usoni, bila kuuliza chochote alimshika mkono na kumuambia aingie ndani ya gari.

Suzana naye alifanya hivyo bila kuuliza maswali kisha gari likatimua mbio wakielekea nyumbani kwa akina Black.

                                  *********************************

Mr Herman alibeba dumu la mafuta ya petrol tayari kwa kuchoma moto kila kitu ambacho kilisalia msituni [ale baada ya kazi kuisha,  aliingia kila chumba na kumwaga mafuta.

Ghalfa aliona kisanduku kidogo kikiwa chini, alikiokota na kukiweka mfukoni kisha akaendelea na kazi yake.

Alimwaga mafuta mahali pote kisha akawasha moto paliteketea na hakuna ushahidi wowote ulibaki, baada ya kazi ile kumalizika alielekea ndani ya gari yake akatoa kisanduku kile na kukiweka kwenye  siti kisha akawasha gari na kuondoka.

Itaendelea..