SEHEMU YA TATU

Mpenzi msomaji badala ya kuweka vipande vinne tumeweka vipande vitano sasa ili kuongeza uhondo wa hadithi yetu, TUNAOMBA RADHI KWA USUMBUFU WOWOTE UTAKAOJITOKEZA ASANTE

Ilipoishia…

Nilijiuliza mwenyewe “mbona bado kama masaa mawili mpaka kufika Dar halafu huyu anasema bado robo saa mmh…!!!” nilitamani kumwamsha Jimmy nimuambie kile nilichokiskia na kuhisi moyoni mwangu nilighairi na kujipa imani kuwa kila kitu kingekuwa sawa. Labda tu ni mahali ambapo alipanga kushukia.

Skruuuuuuh….!!!… Basi letu lilifunga breki ghafla na kuyumba pembeni mwa barabara…. Baada ya dereva kuona magogo yaliyolazwa barabarani…

PAAAAAAH….!!!! Ghafla mlio wa risasi uliozibua masikio yetu, ulioamsha abiria wote waliolala na kuzua taharuki ndani ya sekunde chache ulisikika…!!.

“Wote lala chinii fastaaa….. kabla sijapasua kichwa chako sasa hivi…!” masikio yangu yalikuwa yanauma mno lakini licha ya maumivu hayo yote sauti hii niliisikia barabara kabisa, taratibu nikajumuika na wenzangu ambao tayari walishaanza kulala chini, ndani ya basi lile.

“Maelekezo yetu ni rahisi sana…. Adhabu yake ni kifo endapo utaenda kinyume… ‘simu zote tia ndani ya huu mkoba’..…” hapo nilimuona akipita kijana ambaye alikuwa ameziba uso wake kama ninja akiwa amebeba mkoba mweusi ambao alitumia kukusanya simu zetu zote.

Baada ya dakika kadhaa ndipo akili yangu ikarudi vema, na hapo nikajua kuwa ni kweli tumetekwa!… basi letu limetekwa!!…

Nilinyoosha mkono wangu wa kulia kinyemela nyemela na kuangalia saa yangu ya mkononi nikaona ni saa mbili kasoro, nikajiuliza tumetekwa kweli au? Lakini mbona ni mapema hivi!!…

Jimmy alinivuta karibu naye kisha akanifuta machozi na kuninong’oneza kuwa nisiogope, tayari nilishamkumbuka Mungu wangu!.. tukiwa tumelala chini nilimkumbatia Jimmy kwa uwoga niliokuwa nao huku nikiomba Mungu.

Bila kujua kuwa walikuwa wengi konda wa basi alijaribu kumvamia m’baba yule ambaye alikuwa ameshikilia bastola mkononi mwake purukushani zilianza konda alipambana huku akimwambia Dereva aondoe gari kwani si mahali salama pale.

Dereva alijaribu kuwasha gari na kutaka kuielekeza barabara kuu, Konda alianza kuomba msaada kwani alishaanza kuzidiwa nguvu na yule m’baba..

Nilimwona Jimmy akichomoka kama mshale mahali pale tulipolala, sikujua ni muda gani aliweza kutoa mikono yangu kwani nilikuwa nimemkumbatia kisawasawa alijiunga na wanaume wengine wawili ambao mimi niliwaita Mashujaa wetu, walimchangia m’baba yule na kumsaidia konda katika pambano lile lisilo na matumaini.

PAAAAAAAH..!!!! mlio wa pili ulisikika.. ghafla kukawa kimya.. hakuna ambaye alithubutu hata kusogeza hata ukucha wake, ukimya ulitanda, ni pumzi za kuhema tu ndizo zilisikika muda ule..

Jumaaaa….!! sauti ya Konda iliyojawa na uchungu ilifuatia, nilimsikia akilia kwa uchungu sana, niliinua kichwa changu juu nikaona kioo  cha mbele cha gari kimejaa damu watu wawili wameshafariki akiwemo Dereva ambaye alijaribu kuwasha basi kutuondoa katika dhahama ile.

Machozi ya kwikwi yalizidi kunitoka bila sauti… nilijua tayari mwisho wetu umeshafika, tayari niliona naanza kuchungulia karibu kumfuata mama yangu mzazi aliko niiliumia sana moyoni mwangu.

Wakati huo tayari niliowaita mashujaa wetu walikuwa wameshadhibitiwa viivyo huku konda akilia kwa uchungu wa kumpoteza dereva, ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu pia.

Sikuweza kujua nje ya basi walikuwapo majambazi wangapi, lakini niliweza kushuhudia wawili ambao ndiyo walifyatua risasi zilizompata dereva pamoja na abiria mmoja.

Ghafla wote tuliona mwanga ukimulika kutoka nyuma ya basi letu, niling’amua kuwa lazima ingekuwa basi lingine ambalo tuliliacha nyuma yetu hapo nikahisi labda msaada unaweza kupatikana.

Nikiwa katika dimbwi la mawazo nilimsikia yule baba ambaye alikuwa amekaa pembeni yangu alimuamrisha wenzake kuingia ndani ya basi na kuondoka kwa  haraka, hapo nikagundua kuwa yule hakuwa mtu mzuri kama vile ambavyo nilimuhisi tangu mwanzo.

Watekaji wote waliingia ndani wakiwa na silaha nzito baadhi niliweza kuzitambua ikiwemo bunduki aina ya AK47 pamoja na milipuko ya kurusha kwa mkono niliweza  kujua hizo silaha kwani huwa napenda sana kuangalia filamu za kivita za ughaibuni.

Mkaka mmoja ambaye walimuita black heart, alikuja akamsukuma dereva nje ya basi kisha akawasha na kuondoa basi mahali pale, niliweza kuwahesabu idadi yao kwa haraka, niliweza kufahamu kuwa wapo saba, pamoja na yule m’baba ambaye tulipanda naye kutokea hotelini.

Baada ya gari kuwashwa walituamuru kurudi na kuketi katika siti zetu kama ilivyokuwa mwanzo, na hapo wakang’oa nanga na kutokomea ndani ya msitu.

Hapo akili yangu ilistuka baada ya kuona basi letu likiondolewa kabla hata basi ambalo lilikuwa nyuma yetu halijatufikia, nilibaki na maumivu zaidi moyoni mwangu Jimmy ambaye tayari alisharudi sitini alinikumbatia na kunipa faraja kuwa nisihofu hamna kibaya kitakachonikuta.

Konda alidhibitiwa na asijue la kufanya ndani ya basi mulikuwa munanuka harufu ya kifo tu, kila  mtu alikuwa na majonzi hakuna ambaye alithubutu kuinua mdomo wake kusema neno lolote, wanaume sita tu ndio waliokuwa wamesimama huku wamejiifunga minyororo ya risasi na mabegani mwao wamebeba bunduka kama vile wanaandaliwa kwenda vitani.

Basi letu lilitokomezwa ndani ya msitu sikuweza kutambua ni eneo gani lakini nilijua tu kuwa tayari Morogoro tulikuwa tumeshapita na hiyo ilikuwa tayari ni safari ya kuingia Dar es salaam, sikujua ni msitu gani ule ambao tuliingizwa, nilibaki kimya kusubiri nini kinajiri.

Basi letu lilitembea kiasi cha kilometa kama tatu na nusu hivi ndani ya msitu tayari hapo ilishakuwa imefika saa nne kasoro robo hakuna hata aliyeingiwa na chembe ya usingizi, wala kupatwa na haja wala kusikia njaa wote tulikuwa kimya moyoni mwangu nilikuwa nikipiga maombi ya kila namna kumuomba Mungu atunusuru katika janga hili.

Mikononi mwangu sikuweza kuacha begi ambalo nilitunza kisanduku nilichopewa na mama yangu, nilikitunza katika misukosuko yote hiyo ili nisije kupoteza siri zilizomo ndani yake ambazo nilitakiwa kuzijua.

Basi lilisimama katikati ya msitu kisha abiria wote tukaamrishwa kushuka na kupanga mstari mbele ya basi ambapo kulikuwa na mwanga wa taa za basi, wote tulifanya hivyo bila kupinga kwani kilichopo muhimu ilikuwa ni uhai wetu tu.

Kisanduku changu nilikifunga kwa mkanda kiunoni kwangu ili nisiweze kukiacha mahali popote niendapo kwani hakuna ambaye aliruhusiwa kutoka na kitu chochote ndani ya basi, niliwaona watekaji wale wakiiingia ndani ya basi na kukusanya kila kilicho kizuri kwao,  nilimuona black heart amekichukua mkoba wangu na kuuweka kwenye mabegi yao, niliumia sana.

Tayari akilini mwangu nilishaweza kumkariri black heart kwani ndiye niliyekuwa nikimsikia tangu mwanzo wa safari mpaka saa ile.

Lori moja lilikuja mpaka pale tulipo lilibeba mabegi yetu na vifaa vyote ambavyo ni vya thamani kisha likaondoka na kutokomea mahali tusikokujua wakati huo pesa zangu zote zilikuwa zimeshakwenda na watekaji wale, nilianza kuona mambo yanakuwa mazito kwa upande wangu.

Nilimuangalia Jimmy ambaye kwa wakati huo alikuwa amekaa upande tofauti na mimi baada ya waume na wake kutenganishwa.

Hakuna kitu chochote kilibaki ndani ya lile basi zaidi ya vitu tu visivyo na thamani, na alama za damudamu tu…  aliitwa Jemedari na kuambiwa afanye kazi yake, ukimuangalia alikuwa ni kijana wa makamu mzuri kwa sura lakini roho yake ilionekana kuwa ni chafu mno.

Alikuja mahali ambapo tulikuwa tumesimama  abiria wote kisha akatuambia kuwa, abiria wote wenye umri wa miaka 45 kushuka chini wajipange mstari mmoja tofauti na abiria ambao walikuwa na umri wa miaka 46 na kuendelea..

Tukafanya hivyo hakuna ambaye  alipinga, karibu robo tatu ya basi zima tulikuwa abiria ambao tupo chini ya miaka 45, hila abiria 15 tu ambapo ndani yake wazee walikuwa watano waliwekwa kwenye kundi lao, mbali kidogo nasi.

Sisi ambao tulikuwa na miaka chini ya 45 tulifungwa minyororo mizito miguuni na mikononi kama vile watumwa wa kihistoria, kiasi ambacho hata mmoja wetu asingelijaribu kuvunja na  kutoroka, wakati huo nilifungwa mbali na Jimmy na sikuweza kuwasiliana na kwa mdomo wala ishara.

Mzee mmoja aliamua  kujitoa muhanga kwa kumfuata yule baba ambaye tulikuwa nae kwenye safari, kisha akamuambia “mwanangu nini munahitaji tuwapatie tafadhali…” baba yule alimuangalia jicho baya kisha akamsukuma pembeni na kumwambia asubiri zamu yake inakuja.

Tuliamrishwa kusonga mbele na kumfuata black heart, tukiwa katika msururu na tumefungwa minyororo miguuni mwetu, pembeni walikuwa watekaji wengine ambao waliachwa na lori ili kuongeza nguvu.

Safari yetu iliendelea katika msitu ule ambao ulikuwa na kiza kinene wakati huo tayari ilikuwa imeshatimu saa tano na zoezi  la kututenganisha lilikuwa limedumu kwa muda wa  dakika kumi na tano tu.

Hatua chache mbele tulisikia milio mingi ya risasi, nilipogeuka nyuma niliona miili ya wale wazee na wenzetu ambao walikuwa na zaidi ya miaka 46 na kuendelea ikiwa imelala chini inavuja damu,”wameuawa…..!!!” nilijiuliza mwenyewe nafsini mwangu, mwili wangu ulitetemeka nikajua huku tuendako hakuna usalama tena.

Itaendelea..

Tunakuomba kujiunga nasi ili uwe wa kwanza kupata hadithi na habari zetu kemkem kila mara tunapozichapisha