NA GLORY OLOMI

Ewe Msichana!. Huna haja ya kukaa kimya inapotokea umefanyiwa ukatili wa kijinsia au hata wa kisaikolojia, ni haki yako kusimama na kupaza sauti kumaliza vitendo hivi. KUMBUKA: MWILI WAKO, MAAMUZI YAKO, THAMANI YAKO!.

NI 2017, mwezi wa tisa sasa matatizo ya kifua yaliyonitesa kwa mwaka mzima yameshika hatamu ilibidi nirudi hospitali kwa uchunguzi zaidi. shangazi alinielekeza kwa daktari bingwa, daktari aliyeuamini na kumsifia, nami sikuwa na budi kufunga safari kwenda kumuona daktari huyo, nilitembea kwa furaha kuelekea hospitali nikijua kabisa leo ni siku ya kupata suluhu ya tatizo hili la kifua kubana na kukohoa bila kikomo.

Nilipofika mapokezi, nilitaja jina la daktari ninayetaka kumwona, na kwenda kusubiri zamu yangu nje ya ofisi yake. Tulikuwapo wengi tuliosubiri huduma yake, na wengi walikuwa ni watu wazima isipokuwa mimi tuu.

Nilijawa tumaini na ujasiri nilipoitwa kuingia katika chumba cha daktari, katika uchunguzi wake, ilitakiwa nifanyiwe vipimo vya x-ray pamoja na kuangaliwa moyo. Nilienda chumba cha x-ray na kisha kurudi kwa daktari kwa ajili ya vipimo vya moyo.

Kipimo hicho kilihusisha kupaka mafuta kwenye kifua karibu na matiti yangu na kupitisha mashine ndogo ya kitaalamu kuangalia moyo. Hivyo ilinibidi kuvua nguo yangu ya juu, nami nilifanya hivyo mafuta yalipakwa na mashine ikaanza kupitishwa taratibu. Ilianza kitaalamu, kidaktari, baada ya muda ikaanza kuwa ya ajabu, daktari akaanza uliza maswali binafsi yasiyokuwa sawa kumuuliza mgonjwa, una boyfriend?, umeolewa?, unajisikiaje mashine inapopita katikati ya kifua chako mrembo?. Ghafla mashine ikawekwa chini na mikono yake ikageuka kuwa mashine ya kuupapasa mwili wangu, nikashtuka niliinuka kitandani na kumwambia kama vipimo vimeisha naomba sasa nirudi nyumbani

Moyoni niliumia sana, huyu ni daktari niliyemwamini, daktari ambaye hata nyumbani wanamwamini….. Lakini ona alichokifanya kwangu. Nilijisikia vibaya na kuona labda makosa yalikua yangu, niliwaza sana juu ya tukio hili na hatimaye niliadhimia kurudi nyumbani. Sikuweza kumweleza mtu yeyote kitendo kile, niliogopa na kuona aibu kwani nilidhani nipo mwenyewe aliyewahi kufanyiwa kitendo cha udhalilishaji kama kile.

Ni kilio kwa wasichana wadogo na wanawake kwa kile ambacho wanakipitia kila siku matendo yafanywayo na wakubwa wetu, wanaume tunaowaheshimu na kuwaangalia, Kati ya wanawake 10, 9 wamepitia ukatili wa kingono, kushikwa sehemu za mwili bila ridhaa na ukatili wa kisaikolojia, kudhalilishwa kwa maneno vitendo na ishara, kusingiziwa ama kuaibishwa. Haya hutokea sehemu yeyote, hospitalini, ofisini, kwenye daladala, nyumbani hata katika mikusanyiko ya watu.

Muhtasari wa haki za binadamu mwaka 2018 unataja Haki zilizovunjwa zaidi kwa mwaka 2018;

  • Uhuru dhidi ya Ukatili Ukatili wa kingono dhidi ya watoto
  • Ukatili wa kimwili dhidi ya watoto
  • Ukatili wa kiuchumi dhidi ya wanawake
  • Ukatili wa kimwili na kisaikolojia dhidi ya wanawake

Vitendo hivi hufanywa na wanaume walio karibu yetu au hata wale tusiowafahamu kabisa huko mtaani, hufanyika kwa siri au katika hadhara. Watendaji wa vitendo hivi hutokomea pasi na kujulikana na watendwa kuachwa na vidonda vya kimwili na kihisia.

Labda waweza sema “wanawake wanajipeleka katika hali hizo, wameyataka wenyewe”, usichokijua ni kwamba, idadi ya wahanga ambao wanafanyiwa ukatili huu wa kingono na kisaikolojia ni mara kumi zaidi ya hao wanaotaka wenyewe. Kinachofanya uwaone hao wanaopenda ni zaidi ni kwasababu wao wanayaongelea kwa watu na hili kundi lingine wanashindwa kabisa kuzungumza yanayowakuta hivyo huumia na kubaki nayo moyoni.

Hatuna sauti tuwezayo kuzungumzia, hatuna mazingira mazuri kuzungumza na wazazi wetu, ndugu, jamaa na rafiki zetu. Hatuna nyenzo za kutumia tunapokutana na hali kama hii. ukisema unaambiwa “umeyataka”, “unasingizia watu”, “unasema uongo” au mbaya zaidi “Na yeye ni binadamu ana mapungufu yake”. Imani zetu zinatetereka juu ya huu msemo “mwanaume ni mlinzi”, “mwanaume ni nguzo”. Huyu mwanaume aliyetakiwa kuwa mlinzi ananikatili na kunivunja moyo. Badala ya kunilinda nnanivamia!!.

Hivi visa ni vingi mno kuthibitisha hili muulize msichana au mwanamke aliyekaribu nawe binafsi nina shuhuda tatu kubwa zilizokaa kichwani mwangu, yaliyonikuta mimi… Ifike mahala kama jamiii tubadilike…. Enyi vijana wababa na wazee mnaosoma makala hii mtuheshimu na MUHESHIMU MIILI YETU NA MAAMUZI YETU.

Ewe Msichana!. Huna haja ya kukaa kimya inapotokea umefanyiwa ukatili wa kijinsia au hata wa kisaikolojia, ni haki yako kusimama na kupaza sauti kumaliza vitendo hivi. KUMBUKA: MWILI WAKO, MAAMUZI YAKO, THAMANI YAKO!.