ULIMWENGU tunaoishi umekumbwa na majanga mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa yameacha makovu, makovu ambayo ni vigumu kuyafuta ama kuyasahau, mamilioni ya watu wamepoteza maisha kutokana na magonjwa, matetemeko ya ardhi, Tsunami na majanga mengine mengi yanayoendelea kuupiga ulimwengu.

Leo tutaangazia magonjwa ya mlipuko ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha athari nyingi tangu kuanza kwa ulimwengu mpaka hivi sasa, wanadamu tunasumbuliwa na covid-19. 

430 K.K: Athens

Huu ulikuwa ugonjwa wa awali kabisa kuwahi kurekodiwa katika historia ya magonjwa  yanayoambukiza na kuenea kwa kasi sana. Ugonjwa huu ulienea huko Athens katika kipindi cha pili cha vita ya Peloponnesia kisha madhara yake yakasambaa mpaka kufikia katika falme za Kigiriki na Mediterania ya Mashariki.

Watunzaji wa kumbukumbuku wanasema kuwa ugonjwa huu ulianzia huko Kusini mwa Ethiopia, ambako ulisambaa kupitia Misri na Libya kisha ukaikumba bahari ya Mediterania na kuingia Persia na hatimaye kufika Ugiriki.

Ugonjwa huu unakadiriwa kuua watu 250,000 hadi 300,000 katika karne ya tano huku waathirika wakubwa wakiwa ni Athens, dalili zake ni: Homa, Kushikwa na kiu kikali, ngozi kuwa na rangi nyekundu pamoja na kuwa na damudamu katika koromeo na ulimi.

165 A.D: Ugonjwa wa Atonine

Ugonjwa wa Pigo la Antonine ulionekana kuanza kama ugonjwa wa Surua, pia unasemekana ulianzia huko Hani kisha ukasambaa mpaka Ujerumani, baada ya ugonjwa huu kuipiga Ujerumani ukasambaa tena Roma kupitia Jeshi lake ambalo lilikuwa Ujerumani kwa wakati huo.

Ugonjwa huu una dalili kama vile; Homa kali, kukauka koo na kuharisha pigo hili lilidumu mpaka miaka ya 180 A.D huku ikidaiwa kuwa mpaka Mtawala Marcus Aurelius aliugua ugonjwa huo.

250 A.D: Ugonjwa wa Cyprian

Ugonjwa huu ulipewa jina kutokana na mgonjwa wa kwanza kuumwa ambaye alikuwa ni Askofu wa Kikristo wa jimbo la Carthage, mgonjwa aliweza kutambuliwa kwa kuwa na dalili kama vile; kuhara, kutapika, kuwa na vidonda shingoni na homa kali.

Walioko mijini waliamua kuhama kwa nia ya kuukimbia ugonjwa badala yake ndiyo kwanza ni kama walikuwa wanausambaza zaidi katika maeneo ya vijijini.

Inasemekana kuwa ugonjwa huu ulianzia Ethiopia, kisha ukasambaa kupitia kaskazini mwa Afrika na hatimaye kufika katika ngome za Roma, haikukomea hapo tu ugonjwa huu ulifika mpaka Misri.

Karne ya 11: Ukoma

Haijalishi ni miaka mingapi imepita bado Ukoma ni tishio kubwa masikioni mwa wengi, Ukoma ulienea sana katika mataifa ya Ulaya na kusababisha kujengwa kwa kambi nyingi ili kuweza kuzuia ongezeko la wagonjwa wa ukoma.

Pia unajulikana kama Ugonjwa wa Hansen, ugonjwa huu uliosababishwa na bakteria ambao taratibu hula viungo vya mwanadamu na kumwacha na mapungufu katika viungo vyake uliaminika kama laana kutoka kwa Mungu kwenda kwa familia zinazokosea hapa duniani.

Shirika la Afya Duniani WHO limeripoti kuwa hadi leo hii bado ugonjwa huu upo na maambukizi yake hufikia mpaka watu 200,000 kwa mwaka.

1817: Kipindupindu cha Kwanza

Kipindupindu cha kwanza kiliua watu zaidi ya milioni moja, ugonjwa wa huu wa mlipuko kwa mara ya kwanza ulipima huko Urusi, kati ya njia ambazo ugonjwa huu uliambukiza kwa haraka ni kupitia maji machafu yaliyoambatana na kinyesi cha muathirika, au chakula kilichoathiriwa.

Ugonjwa huu pia ulisambazwa na wanajeshi wa Uingereza ambao walipitia India na kuambukiza mamilioni ya Wahindi, Jeshi hilo pia lilisambaza ugonjwa huu mpaka Hispania, Africa, Indonesia, China, Japani, Italy Germany na America na huko kote watu 150, 000 zaidi walipoteza maisha. Chanjo yake ilipatikana 1885 ila bado ugonjwa huu unaendelea kuwa tishio.

1889: Mafua ya Kirusi

Mafua ya kwanza ambayo yaliweka historia kubwa katika uso wa dunia, yalianzia huko Siberia na Kazakhstan, kisha yakasambaa mpaka Moscow na kufika mpaka Finland na Poland na kisha kusambaa Ulaya yote.

Mwaka uliofuata ilivuka mipaka na kusambaa mpaka Amerika ya Kaskazini na Afrika, na mwishoni mwa mwaka 1890 watu 360,000 walipoteza maisha.

1918: Mafua ya Kihispania

Mafua makali ambayo yalipelekea vifo vya watu Milioni 50 dunia nzima, mafua haya awali yaligundulika huko Ulaya, Marekani na baadhi ya maeneo kutoka Asia kabla ya kusambaa dunia nzima.

Kwa kipindi hiko hakukuwa na tiba wa chanjo yoyote ya kutibu ugonjwa huu baadhi ya vyanzo vinaripoti kuwa ugonjwa huu ulianzia katika jiji la Madrid huko Hispania katika msimu wa baridi mwaka 1918.

Mpaka kufikia mwezi Oktoba maelfu ya Waamerika walipoteza maisha mpaka sehemu za kuhifadhia wafu zikawa chache, lakini ilipofika majira ya joto mwaka 1919 gonjwa hilo likatoweka baada ya walioambukizwa wengi kufariki na waliobaki kupata kinga za mwili.

1957: Mafua ya Asia

Mafua haya yalianzia huko Hong Kong na hatimaye kuenea China nzima, kisha kusambaa nje ya mipaka ya China na kuingia Marekani. Ndani ya miezi sita Mafua ya Asia yaliweza kusambaa mpaka Uingereza na watu 14,000 walipoteza maisha.

Ugonjwa huu ulisababisha tena vifo vingi mwanzoni mwa mwaka 1958 ambapo watu milioni 1.1 walipoteza maisha duniani kote huku vifo 116,000 vikiripotiwa kutokea Marekani pekee, chanjo ya ugonjwa huu iliweza kupatikana.

1981: HIV/AIDS (Ukimwi) 

Hapo mwanzo uligundulika mwaka 1981 kuwa Ukimwi unaharibu kinga ya asili ya mwili na hatimaye kusababisha kifo, dalili kama vile homa, maumivu ya kichwa, kuvimba koo pamoja na vidonda vya kinywa na sehemu za siri vimeripotiwa kuwakumba wagonjwa wa HIV.

AIDS kwa mara ya kwanza ilionekana katika jamii ya mashoga huko Marekani japo inaaminika kuwa chimbuko lake ni kutoka kwa wanyama kama vile Sokwe wa huko Mashariki mwa Afrika katika miaka ya 1920 na ugonjwa huo unaoambukizwa kwa majimaji ya mwilini uliweza kuenea hadi Haiti kati ya miaka ya 1960 pia New York na San Fransisco katika miaka ya 1970.

Majaribio kadhaa yamefanyika lakini bado dawa ya kuponya ugonjwa huu kwa haraka haijapatikana mpaka sasa HIV/AIDs imeua watu milioni 35 duniani kote.

2003: SARS 

Ugonjwa huu unaosababisha maumivu makali katika mfumo wa upumuaji unaaminika kuwa ulianzia kwa popo kisha kuambukizwa kwa paka na hatimaye kuwafikia binadamu huko China kisha kusambaa katika nchi 26 duniani kote na kusababisha maambukizi 8,096 vifo 774.

Dalili za ugonjwa huu ni; shida katika mfumo wa upumuaji, kikohozi kikavu, homa na maumivu ya kichwa na mwili pia husambazwa kwa kikohozi na vitone vya majimaji yatokayo kohoni.

Moja kati ya jitihada zilizotumika ili kuzuia ugonjwa huu ni kuweka watu karantini (kizuizini), tangu hapo ugonjwa uliweza kuzuiwa na virusi vya ugonjwa huo havikuweza kusambaa tena. China ililaumiwa kwa kukaa kimya kuhusu kusambaa kwa ugonjwa huu. kwani nchini kwao ndiko ilionekana kama chimbuko la ugonjwa huo

2019: COVID -19

Machi 11, 2020 Shirika la Afya Duniani lilitangaza kuwa Covid-19 ni ugonjwa wa mlipuko unaonea kwa kasi duniani, ikiwa tayari nchi 114 zimeshaathirika kwa ugonjwa huo na maambukizi zaidi ya 118,000 ndani ya miezi mitatu.

Ugonjwa huo ulitangazwa kuwa unasabbishwa na virusi aina ya corona- aina mpya ya corona ambayo haikuwahi kupatikana hapo awali dalili zake ni: shida katika mfumo wa upuaji, kikohozi, homa ambayo inaweza ksuababisha nimonia na hata kifo kama ilivyo kwa SARS, covid-19 pia huambukizwa kwa majimaji yatokayo mwilini.

Maambukizi ya awali yalitokea China Novemba 17 2019, katika jimbo la Hubei lakini bado haikutambulika mpaka watu nane zaidi walipoambukizwa virusi hivyo mwezi Disemba.

Wengi walijifunza kuhusiana na Covid-19 baada ya daktari wa macho Li Wenliang kukataa agizo la serikali na kutoa tahadhari kwa madaktari wenzake juu ya ugonjwa huo, China iliarifu WHO jambo hilo kisha ikamshutumu Dkt Li kwa uhalifu, mwezi mmoja baadae Dkt Li Wenliang alifariki dunia kwa ugonjwa wa covid-19.

Siku za hivi karibuni Marekani imeruhusu matumizi ya dawa yua Remdesivir ambayo ilitengenezwa kwa ajili ya Ebola kutibu wagonjwa walio mahututi kutokana na covid-19, huku ugonjwa huo ukiwa umesambaa katika nchi zaidi ya 163 duniani

VYANZO

Disease and History by Fredrick C. Cartwright, published by Sutton Publisher 2004

Encyclopedia of Pestilence, Pandemics, and Plague by Ed Joseph, P Bryne published by Greenwood Press  2008

Influenza American Experience

The history website