Kiongozi wa Taifa la Korea Kaskazini, Kim Jong-un ameonekana mbele ya umma kwa mara ya kwanza baada ya kutoonekana kwa takribani siku 20 zilizopita.

Kwa mujibu wa Kikosi cha Habari cha Korea Kaskazini KCNA, kimeripoti kuwa kiongozi huyo ameonekana akikata utepe katika hafla fupi ya ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza mbolea nchini humo.

KCNA wanaongeza kuwa watu waliokuwa katika ufunguzi wa kiwanda hicho walijawa na furaha baada ya kumuona kiongozi wao kwa mara ya kwanza baada ya siku 20 kupita.

Aidha katika ufunguzi huo Bwana Kim alionekana kuamabatana na Maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Korea Kaskazini, akiwemo dada yake Kim Yo Jong.

“Kiongozi wa taifa la Korea Kaskazini akikata utepe katika ufunguzi wa kiwanda cha mbolea kilichopo huko Kaskazini mwa Pyongyang, na watu walioko wakiwa na furaha baada ya kumuona kiongozi huyo akikamilisha moja kati ya mafanikio ya Korea Kaskazini” Walisema KCNA.

Ikumbukwe kuwa kiongozi Kim alitoweka tangu Aprili 12, kufuatiwa na uvumi wa kuwa na matatizo ya kiafya. Pia kutohudhuria katika sherehe ya kuzaliwa kwa babu yake, ambaye ndiye mwanzilishi wa taifa hilo Kim II Sung iliyofanyika tarehe 15 Aprili.

Sherehe hiyo ni moja kati ya sherehe kubwa ambazo hufanywa nchini humo, pia Bwana Kim mara zote huudhuria sherehe hizo, kutokuhudhuria kwake Aprili 15 kumeibua maswali mengi kwa vyombo vya habari pamoja na intelijensia na nchi mbalimbali.

Aidha Sekratari wa Marekani, Mike Pompeo alionekana kama kuchochea uvumi huo kati ya tarehe 29 Aprili baada ya kusema kuwa “Maafisa wa Marekani hawajamwona Kim kwa muda”. Japo intelijensia ya Korea Kusini na China zilikanusha taarifa hizo.