WIZARA ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeripoti watu 36 kati ya 105 waliokuwa na maambukizi ya virusi vya corona wamepona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Akiongea na vyombo vya habari Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema kuwa tayari wagonjwa 36 wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kutokuwa na dalili zozote za ugonjwa wa covid-19.

Aidha Wizara ya Afya imepokea maambukizi mapya saba, na kufanya idadi ya wagonjwa 105, mpaka sasa wagonjwa wote wapo katika vituo vya Kidimni na Shule ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Pia Waziri wa Afya ametoa rai yake kwa wagonjwa waliorudi nyumbani hivi karibuni kuendelea kujitenga kwa muda wa siku 14, ili kupeuka maambukizi yoyote yanaweza kujitokeza katika kipindi hicho huku wataalamu wa afya wakiendelea kuwafuatilia kwa ukaribu.

“Serikali kupitia wizara yake ya afya inandelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huu zinazotolewa mara kwa mara ikiwemo wa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka msongamano hasa mwezi huu wa ramadhani na kuahirisha safari za nje na ndani zisizo na lazima” alisema Bwana Hamad Rashid.

Aidha aliwasihi wananchi wanaojisikia dalili zinazofanana na ugonjwa huu kujitokeza katika vituo vya afya ili kupima covid0-19, au kupiga simu namba 190 pia wananchi kuvaa barakoa muda kwa muda wote wanaokuwa mitaani au katika safari.