SIKU ya Ijumaa Afya ya Umma ya Uingereza imewaomba madaktari na wauguzi wanaofanya kazi mstari wa mbele kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, kufanya kazi hiyo bila kuvaa magauni marefu ya kitabibu pia kutumia vifaa tiba vilivyotumika ili kutibu wagonjwa.

Baadhi ya hospitali ambazo zinatumika kutibu wagonjwa walioathiriwa na covid 19 nchini Uingereza zinatabiriwa kuishiwa vifaa vya kitabibu, ikiwemo magauni marefu kwa ajili ya madaktari na wauguzi kujilinda wafanyapo kazi hiyo.

Madaktari na wauguzi nchini humo wamelalamikia upungufu wa vifaa tiba na vifaa vya kujilinda afya zao utakaojitokeza ndani ya saa 24 had 48 zijazo.

Shirika la Huduma za Afya la Taifa (NHS) limesema kuwa “ugawaji wa vifaa tiba katika hosptali zote umekuwa mgumu, hivyo huduma za vifaa tiba zitaelekezwa katika hospitali ambazo zinatabiriwa kuishiwa vifaa”

Aidha Chama Cha Madaktari cha Uingereza (BMA) kimeonya madaktari kuweka maisha yao rehani ili kusaidia wagonjwa wa corona, Chama hicho kinasema kuwa uamuzi uliochukuliwa na Shirika la afya ya umma unatokana na makosa ya serikali kushindwa kutekeleza ugawaji wa vifaa vya kitabibu.

Mwenyekiti wa chama hicho Dkt Rob Harwood, alisema kuwa “kama imependekezwa kuwa madaktari watumie vifaa vilivyotumika, basi ni lazima hili lichunguzwe kisayansi na ushahidi wa matumizi yake uwe hauna madhara kwa wafanyakazi wa afya”

Mpaka kufikia sasa wahudumu wa afya 50 wamefariki nchini humo katika harakati za kuhudumia wagonjwa wa corona.

Processing…
Success! You're on the list.