June Dalziel Almeida ndilo jina kamili ya mwanamke huyo mgunduzi wa virusi vya corona kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1964

Binti wa dereva wa basi aliyeacha shule akiwa na umri wa miaka 16 kumbukumbu ya kazi yake aliyoifanya miaka zaidi ya 50 iliyopita mpaka leo bado inakumbukwa hasa katika nyakati hizi ambapo dunia ipo katika mapambano dhidi ya janga la virusi ambavyo kwa mara ya kwanza viligunduliwa naye.

Mwanamke huyu alizaliwa Juni mwaka 1930 na kukulia kaskazini mashariki mwa Glascow nchini Scotland

Hadithi ya ugunduzi wake ilianza mara baada ya binti huyo kuacha shule akiwa na umri wa miaka 16 kisha akaamua kwenda kufanya kazi ya ugunduzi wa viashiria vya magonjwa katika zahanati iliyoitwa Glascow Royal Infirmary huko Scotland.

Aliacha kazi katika zahanati hiyo na kuamua kwenda kujiendeleza katika taaluma yake na hapo alihamia London. Mwaka 1954 aliolewa na msanii aliyeitwa Enriques Almeida kutoka Venezuela.

SAFARI YA UTAFITI WAKE

Wanandoa hao pamoja na binti yao walihamia Toronto nchini Canada kwa ajili ya shughuli zao na huko ndiko ambako harakati za ugunduzi wake ziliendelezwa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa masualaya afya George Winter anasema kuwa Dkt Almeida aliamua kujiendeleza ujuzi wake wa kugundua vijidudu vilivyosababisha ugonjwa wa mafua kwa kutumia darubini ya umeme katika taasisi ya kansa Ontario

Bwana Winter anaendelea kusema kuwa kipaji cha mwanamke huyo kiligunduliwa katika hospitali ya St Thomas mjini London huko Uingereza, hospital ambayo imemtibu Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza wakati alipougua Covid 19.

Aliporejea shuleni hapo kama mfanyakazi alishirikiana na Dkt Tyrrell ambaye alikuwa anafanya utafiti wa vijidudu ambavyo vilisababisha mafua ya kawaida.

Sampuli moja iliyotambulika kama B814 iliyotoka katika sehemu ya kunawia maji katika bweni mojawapo la shule hiyo iligundulika kuwa na virusi tofauti na virusi vingine ambavyo vilisababisha mafua.

Ingawa utafiti wa vijidudu hivyo ulifanywa na vijana wakujitolea Dkt Tyrell aliona bora vikaangaliwe katika Darubini ya umeme kwa matokeo bora zaidi, hivyo sampuli hiyo ikatumwa kwa Dkt Almeida.

Baada ya uchunguzi zaidi Dkt Almeida aligundua kuwa virusi hivyo viliweza kusababisha mafua lakini bado havikuweza kufanana na virusi vingine vya mafua vilivyozoeleka na ndio ni kwa mara ya kwanza kubainika katika mwili wa binadamu.

Bwana Winter anasema kuwa ugunduzi huo ulikataliwa kwa mara ya kwanza kwani vilikuwa vijidudu ambavyo havikuwahi kuonekana kabla, pia Dkt Almeida hakuwasilsha picha za vijidudu hivyo.

Bila kusita ugunduzi wa virusi hivyo ukaandikwa kwa mara ya kwanza katika jarida la British Medical Journal mwaka 1965, huku picha ya kile alichokiona iliweza kuchapishwa miaka miwili baadae katika jarida la ‘General Virology’.

Bwana Winter anaiambia BBC kuwa Dkt Almeida na Dkt Tyrell wakishirikiana na Prof Tony Waterson, mkuu wa Chuo cha St Thomas waliamua kuvipa virusi hivyo jina la corona kutokana na muonekano wake uko sawa na taji.

Dkt Almeida aliweza kutunukiwa shahada ya udaktari wa afya.

Ukiachana na ujuzi wa kitabibu Dkt Almeida alikuwa mwalimu wa Yoga, Dkt June Almeida alifariki mwaka 2007 akiwa na miaka 77 ugunduzi alioufanya bado umakumbukwa sana katika kipindi hiki dunia imejawa na majonzi kutokana na vifo vinayosababishwa na ugonjwa covid 19, huku tiba ya ugonjwa huu ikiwa bado ni pasua kichwa kwa madaktari,

Labda angelikuwepo mpaka leo basi huenda angeshiriki vyema katika utafiti wa tiba ya virusi hivi kwani Prof Hugh Pennington anasema kuwa Wachina walitumia njia za Dkt Almeida ili kuweza kugundua covid 19.

Processing…
Success! You're on the list.