MAMLAKA ya anga nchini Tanzania imefuta usafiri wa ndege zote za abiria wa kimataifa kuingia nchini humo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na shirika la usafiri wa anga Tanzania (TCAA) limetangaza kusimamisha usafiri wa ndege zinazobeba abiria wa kimataifa, huku shirika hilo likiruhusu ndege zinazobeba mizigo tu kuingia nchini humo.

Aidha shirika hilo limesema kuwa ndege zinazobeba mizigo zitaruhusiwa kuingia zikiwa na rubani na wahudumu tu ambapo nao watahitajika kukaa karantini kwa gharama zao binafsi.

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas ameandika kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa hiyo ni hatua nyingine ya kupambana na ugonjwa wa Covid 19.

Mpaka sasa vifo vitatu vitokanavyo na ugonjwa wa covid 19 vimeripotiwa nchini humo, idadi ya maambukizi ya corona inazidi kupanda mpaka kufikia watu 32 huku maeneo yaliyoathirika sana yakitajwa kuwa ni Zanzibar, Arusha Dar es salaam na Mwanza.