MAMLAKA za Afya nchini Tanzania zimethibitisha kuwepo kwa maambukizi mapya 17 ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, huku ikitajwa kuwa Tanzania visiwani ina idadi ya wagonjwa watatu kati ya hao 17.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Bi Ummy Mwalimu ametangaza maambukizi mapya kwa watu 14 kutoka Tanzania Bara na watu watatu kutoka Visiwani, idadi ya watu walioambukizwa nchini Tanzania kwa sasa ni 49

Taarifa kutoka Wizara ya Afya nchini Tanzania zinasema kuwa raia hao ni wa Tanzania ambao hawana historia ya kusafiri kwenda nje ya nchi hivi karibuni. Watu 13 kati ya waliombukizwa ni wakazi wa jijini Dar es salaam na mmoja ni mkazi wa Arusha.

Mpaka sasa jiji la Dar es salaam lenye wagonjwa 32 linaonekana kushambuliwa zaidi na ugonjwa huo ukilinganisha na maeneo mengine nchini humo kama vile Zanzibar (12), Arusha (3), Kagera (1) na Mwanza (1).

Hivi karibuni serikali ya Tanzania imeongeza baadhi ya makatazo ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiriana na ugonjwa huu wa covid 19. Mojawapo ya makatazo yaliyoongezwa ni kuwekwa kwa marufuku ya ndege za kimataifa za abiria kuingia nchini.