“Hivi ni kweli mapenzi hutoweka baada kuingia katika ndoa?, Jambo gani ambalo hufanya wanandoa wengi kuhisi kuwa mapenzi yao yamekwisha mara baada ya kuingia katika ndoa?”

Bwana mmoja huko Dallas, Marekani amewahi kufunga Ndoa mara tatu katika nyakati tofauti tofauti lakini zote hazikuwahi kudumu, hivyo akaamua kwenda kumwona Daktari Carry Chapman mtaalamu na mshauri wa masuala ya mahusiano, ili amueleze tatizo lake huenda akapatiwa ufumbuzi.

Alipofika akapewa nafasi ya kuonana na Daktari Chapman kabla ya kupata ruhusa ya kuongea, kwa shauku kubwa Bwana yule akasema Daktari mara zote nimetafuta nafasi ya kuonana na wewe ili nikuulize kwanini mapenzi hutoweka baada tu ya kuingia katika ndoa?, Mapenzi yanapatwa na na nini hasa? aliongezea yule bwana.

Dk Chapman hakumuelewa Bwana yule ndipo akamuuliza “una maana gani kusema hivyo?” Yule bwana akaendelea kwa kusema kuwa, nimewahi kufunga ndoa mara tatu katika nyakati tofauti, lakini zote hazikudumu, ya kwanza ilikaa kwa miaka kumi tu, ya pili ikawa kwa miaka mitano tu na ya tatu ikawa kwa miaka miwili tu, ijapokuwa mara zote nilifahamu kuwa nilikuwa mwaminifu kwa ndoa yangu sikuwahi hata mara moja kuchepuka nje ya ndoa yangu.

Dk Chapman alishangaa kidogo kisha akamuomba aendelee, Yule bwana akaendelea kwa kusema kuwa, ndoa yangu ya kwanza tuliweza kuwa na miaka minne ya mwanzo ya furaha lakini baada ya kupata mtoto wa kwanza hapo ndipo mambo yalipoharibika, hapakuwa na mapenzi tena, nilipomuuliza alisema kuwa “huwezi ona jinsi gani napata tabu kumlea mtoto kwanini usinisaidie” lakini mara zote nilijaribu kumsaidia kulea mtoto wetu lakini bado hakuwahi kuniona wa thamani tena,

Ndoa yangu ya mwisho, mwanzoni upendo ulikuwa mkubwa sana tulipendana mno, nami niliamini kuwa tungeishi siku zote japo haikuwa hivyo baada tu ya kuingia katika ndoa. Hata hivyo siku zote nilimueleza jinsi gani nilimpenda, jinsi gani alivyokuwa mrembo pia mwenye kunivutia mara zote, nilimweleza siku zote jinsi gani nilijivunia kuitwa mume wake.

Soma Makala za kusisimua kutoka Mira Magazine

Lakini miezi michache baada ya ndoa, alianza kubadilika na kuniambia kuwa sina mapenzi ya dhati kwake, alisema kuwa simpendi kama ilivyokuwa mwanzo, alianza kuwa mkali katika mambo madogo kama vile simsaidii kazi za nyumbani simeletei mboga kama ilivyokuwa mwanzo, toka hapo hakuwahi tena kuniamini alianza kunihisi kuwa nimeanza kuishi na wanawake wengine lakini kwa ukweli sikuwa na mwanamke mwingine zaidi yake, hali hiyo iliendelea mpaka tulipoachana.

Hivyo Dk katika haya yote niliyopitia swali langu bado halipati uvumbuzi, nini hutokea katika mapenzi baada ya kufunga ndoa?, kwanini mapenzi mara zote yanatoweka kwangu baada ya kufunga Ndoa?.

Kiukweli swali ambalo yule bwana anajiuliza ni swali ambalo wanandoa wengi wanaooa/kuolewa kisha wakaachana huwa wanajiuliza, wengine pia huanza kuhisi kuwa labda hawakuwa na muda wa kutosha kutambuana katika mwenendo wa tabia zao.

Mapenzi ni jambo la hisia hivyo shauku ya kuwa na mapenzi bora baada ya ndoa lazima ijengwe katika akili na mioyo yetu wenyewe,

Kwanini ni wanandoa wachache sana ambao hufanikiwa kustawisha ndoa yao licha ya msaada wanaoupata kutoka kwa wataalam, vitabuni, katika majarida mbalimbali na magazeti makubwa juu ya siri za kustawisha upendo baada ya ndoa?

Ulishawahi kujiuliza ni kipi kinawafanya wanandoa kuhudhuria semina za ndoa kwa pamoja, kusoma maudhui ya kujenga ndoa kwa pamoja lakini bado wanashindwa kuyatekeleza maudhui hayo kwa kiasi cha kuipa uhai ndoa yao?

Ni muhimu kujifunza lugha ya upendo ambayo mwenza wako anaitumia

Ingawa mapenzi ni jambo la hisia, hisia hizi haziwezi kufahamika kwa mwenza wako mpaka pale utakapozifikisha/ kuziweka wazi mbele yake. Ni vizuri kutambua lugha ambayo mpenzi wako ataielewa pale utakapoeleza hisia zako kwake, wenza wengi huongea lugha tofauti tofauti za upendo.

Katika sayansi ya lugha (linguistic) kila mmoja hujifunza lugha ambayo hukutana nayo katika mazingira anayolelewa na hiyo huwa lugha ya kwanza, yaweza kuwa kichina, kiswahili ama kiingereza. kadri tunavyozidi kukua tunaanza kujifunza lugha tofauti na zile ambazo tunazifahamu, ili kuweza kupata mawasiliano kwa watu ambao hawatumii lugha sawa na ile tuliyozaliwa nayo.

Vivyo hivyo katika mapenzi kila mmoja wetu ana lugha yake ambayo ni kama lugha mama, lugha yako na lugha ya mwenza wako zaweza kuwa tofauti kama ilivyo kwa lugha ya kichina na kiingereza, Hivyo mwenza wako hawezi kukuelewa endapo utaelezea hisia zako kwa lugha ya kiingereza hali ya kuwa yeye anaelewa lugha ya kichina.

Je ulishawahi kuona watu wa kabila, Utaifa na lugha tofauti wakidumu katika mapenzi? umewahi kujiuliza ni lugha gani huwa wanatumia kwa mawasiliano yao?.

Asilimia kubwa ya lugha zetu huundwa kuwa maneno na ishara, lakini lugha za mapenzi huundwa kwa matendo yaliyobeba maelezo ya hisia huru

Daniel filbert

Hapo awali yule Bwana aliyepoteza ndoa tatu alieleza jinsi alivyoonyesha upendo wake kwa wenza wake, ameeleza kuwa katika ndoa yake ya tatu mara zote alimueleza mpenzi wake jinsi gani alimpenda, jinsi gani alivyokuwa mzuri na alijivunia kuitwa mumewe, lakini bado mwanamke hakumuelewa na alimtuhumu kuwa anatoka nje ya ndoa hatimaye ndoa yao ikavunjika,

Hapo tunaweza kujifunza kuwa mapenzi hayawezi kuwa na uhai katika maneno pekee, ndio maana yule mwanamke alimwambia kuwa tangu tufunge ndoa umebadilika, umeacha kuniletea mboga kama zamani, hunisaidii kazi kama ilivyokuwa mwanzo. Jambo hili linatufunza kuwa mapenzi huishi katika matendo ya hisia na si maneno tu

Hisia za mapenzi hufikishwa kupitia lugha mbalimbali hapo mwanzo kabla ya kufunga ndoa, yule bwana alielezea hisia za mapenzi yake kwa mwenza wake kupitia lugha ya (tabia na matendo) hivyo ikawa rahisi kwa mwenza wake kutambua lugha hiyo na kuweka akilini mwake.

Baada ya kufunga ndoa bwana yule alibadilisha lugha na kuhamia katika lugha ya maneno, maneno ambayo ndani yake alionesha dhati (sincere) ya mapenzi yake kwa mwenza wake, na hapo ndipo ikawa mwanzo wa matatizo, kwani huenda mwenza wake bado aliendelea kutafuta upendo wa kweli katika matendo na tabia ya mumewe lakini hakuweza kuona kwa kuwa tayari mume alishahamisha upendo huo na kuhamia katika maneno tu bila tabia na vitendo. Na hivyo akahisi kuwa hapendwi kabisa.

Ukweli ni kwamba kabla ya ndoa wengi wetu huelezea hisia zetu za mapenzi kwa wenza wetu kupitia lugha mbalimbali, lakini tunapoingia katika ndoa lugha zetu hubadilika na kuleta hisia tofauti kwa wenza wetu (kama ilivyokuwa kwa yule mke wa tatu), tunaacha kueleza hisia zetu katika matendo na tabia zetu kisha tunaeleza kupitia maneno yetu ambayo tunayabebesha sifa za ukweli na uwazi, kutamka kuwa unampenda haitoshi jaribu kumuonyesha huo upendo upo vipi.