MASTAA baranI Ulaya wamejitokeza kwa wingi katika kuchangia fedha na vifaa ili kusaidia kupambana na virusi vya Corona, baadhi yao wakiwa wametoa msaada huo kwa mashirika binafsi yanayopambana na virusi hivyo.

Huku wengi wao wakiwa wamejikita katika kuchangia vifaa kama vile barakoa zinazosaidia wahudumu wa afya katika mashirika na vituo vya afya vinavyopigana vita dhidi ya COVID-19.

Hawa ni baadhi ya mastaa ambao wamejitokeza kutoa michango yao ili kupambana na virusi vya Corona.

Angelina Jolie

Muigizaji mkongwe wa filamu Hollywood, Angelina Jolie ametoa kiasi cha Dola za kimarekani Milioni Moja, ili kusaidia watoto wasio na chakula na makazi katika kipindi hiki cha kupambana na COVID-19.

Machi 25, 2020 Kinara huyo wa tuzo za Oscar aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa “Katika wiki hizi zaidi ya watoto bilioni moja duniani kote hawapo shule kutokana na virusi vya Corona”

“Watoto wengi hutegemea lishe na uangalifu wanaoupata wakiwa shule,  Karibia watoto milioni 22 kutoka America wanategemea chakula kutoka shule” aliongeza nyota huyo.

Kylie Jenner 

Bilionea mdogo duniani, Kylie Jenner amechangia kwa nafasi yake kiasi cha Dola za kimarekani milioni moja huko Los Angeles kwa ajili ya kununuliwa kwa vifaa ambavyo vitatumika kukinga wahudumu wa afya wanaopambana dhidi ya virusi vya Corona.

Tabibu binafsi wa bilionea huyo Dr Thais Aliabadi ameeleza hisia zake juu ya msaada alioutoa Jenner,  kupitia ukurasa wake wa instagram aliandika kuwa “Imetimia haja yangu kupata barakoa kwa ajili ya wafanyakazi wetu wa afya, na leo ndoto zangu zimekuwa kweli kwasababu ya mchango wa Kylie”

Rihanna

Siku mbili kabla ya Kylie Jenner kutoa msaada wake, mwanamuziki na Kinara wa tuzo za Grammy, Rihanna Fenty akishirikiana na Clara Lionel Foundation ametoa mchango wa Dola za kimarekani milioni tano, ili kusaidia mapambano dhidi ya COVID-19.

Fedha hizo zimegawanywa kwa baadhi ya mashirika binafasi kama Direct Relief, Feeding America na Partners in Health ambayo yanajihusisha na kupambana na virusi vya Corona.

Taylor Swift

Mkongwe huyo wa muziki wa Pop, ametoa kimya kimya kiasi cha zaidi ya $3,000 kuwasaidia watu ambao wamehitaji kulipa bili za makazi, barakoa pamoja na mahitaji yote ya lazima katika kipindi hiki cha COVID-19.

Ingawa Taylor Swift hakuweka bayana kuhusu mchango alioutoa, baadhi ya mashabiki zake na wanufaika wa mchango huo wameweka machapisho katika kurasa za Instagram wakimshukuru Nyota huyo kwa mchango wake.

Ariana Grande

Nyota wa wimbo wa ‘Side to Side’, Ariana Grande amekuwa akitoa misaada mfululizo kwa mashabiki zake ambao wamewekwa kizuizini kutokana na ugonjwa wa Corona, Ariana amekuwa akiutumia mtandao wa Venmo kutuma fedha fedha kwa mashabiki zake ili kuwasaidia katika kupata mahitaji yaliyo ya lazima kwa kipindi hiki.