NGULI wa muziki wa Afro Jazz, Manu Dibango raia wa Cameroon amefariki dunia jijini Paris nchini Ufaransa baada ya kupatwa na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Mwanamuziki huyo ambaye alijizolea umaarufu mkubwa  kwa uwezo wake wa kupuliza saxofoni amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86, taarifa za msiba wake zimeripotiwa katika ukurasa wake wa Facebook

“Ni kwa machungu na huzuni kubwa kutangaza kwamba Dibango amefariki dunia leo tarehe 24/03/2020 akiwa na umri wa miaka 86”

Baadhi ya wanamuziki wakongwe barani Afrika wameelezea machungu yao kufuatia msiba wa nguli mwenzao Dibango.

Kupitia ukurasa wake wa twitter nguli wa muziki Kidjo ameweka video  ikimuonesha akifanya mazoezi ya uimbaji wa Soul Makossa akiwa na marehemu Dibango miezi miwili iliyopita.

Katika chapisho hilo Kidjo ameambatanisha  maneno yanayoashiria  huzuni  aliyonayo baada ya kumpoteza mwanamuziki mwenzake

Dibango atakumbukwa kwa jitihada zake za kufanya mapinduzi makubwa  katika muziki wa Afrika,  huku moja kati ya visa visivyoweza kusahaulika ni kitendo cha Dibango kudai hakimiliki kutoka kwa aliyekuwa mfalme wa Pop duniani marehemu Michael Jackson baada ya  kutumia vionjo vya wimbo wa Soul Makossa wa Dibango  katika albamu ya Thriller mwaka 2009.

Nguli huyo  ameacha  watoto watatu wakiwamo  Georgia Dibango, Marva Dibango na Michael Dibango

Miramagazine inaungana na familia ya Dibango,  ndugu, jamaa na wadau wote  wa muziki wa Afrika katika kipindi chote cha maombolezo.