WARREN Edward Buffett inawezekana kuwa ni mara yako ya kwanza jina hili kupenya katika masikio yako ama tayari ulishawahi kulisikia hapo awali, Huyu ni moja kati ya wafanyabiashara wakubwa nchini Marekani, Mwekezaji pia ndiye Mwenyekiti wa makampuni ya Berkshire Hathaway aliyezaliwa huko Omaha. Nebraska nchini Marekani mnamo Agosti 30, 1930.

Safari yake ya kuusaka utajiri hapa duniani ilianzia mwaka 1947 akiwa na umri wa miaka 19 mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Biashara cha Columbia.

Leo nimekuletea mambo kumi ambayo Warren Buffet amewahi kuyafanya na tangu hapo basi yamekuwa ya kustaajabisha machoni pa watu.

#1. Maisha yake alipokuwa mdogo.

Kitabu cha The Snowball: Warren Buffet and the Business of Life kilichoandikwa na Alice Schroeder, kinaeleza maisha ya awali na safari nzima ya Warren mpaka alipokuja kufikia ndoto zake za kuwa tajiri mkubwa nchini Marekani Kitabu hiki kimeandika kuwa Buffet akiwa na umri mdogo aliweza kununua Pakiti tano za Chewing Gum, kisha akazifungua na kwenda kubisha hodi katika kila nyumba iliyo mtaani kwao na kuziuza moja moja kwa faida iliyo ndogo sana.

#2. Aliweza kutunza kiasi kikubwa cha fedha akiwa na miaka 16 ($53,000).

Kitabu hicho kinaeleza pia jambo lingine la kustaajabisha kuhusiana na maisha ya Buffet, Katika kipindi ambacho Buffet alihitimu mafunzo ya elimu ya juu (high school) basi alikuwa na uwezo wa kupata kipato kikubwa tena kilichowazidi waalimu wake, hapo akiwa kama meneja wa kiwanda cha kuchakata Karatasi. Pia Kitabu cha Snowball kinaongeza kwa kusema kuwa  Warren aliweza kutunza kiasi cha Dola 53,000 za Kimarekani mpaka alipofikia kumaliza elimu yake ya juu.

#3. Picha yake ya utotoni inayosambaa sana mitandaoni.

Ipo picha maarufu iliyopigwa akiwa na umri mdogo ambapo ilimuonesha Warren akiwa ameshikilia mashine ya kutolea chenji, Warren anasema kuwa mashine hiyo ndiyo iliyomuwezesha kutoa chenji kwa wateja wake hapo alipokuwa na umri mdogo sana

#4. Amewahi kutuma email moja tu katika maisha yake.

Alipofanyiwa mahojiano na Pierce Morgan kuhusiana na matumizi yake ya teknolojia katika maisha yake ya kibiashara, Warren Buffet alijibu kuwa “Nimetuma barua pepe
(email) moja tu katika maisha yangu” aliendelea kwa kusema kuwa “niliituma kwa Jeff Raikes wa kiwanda cha Microsoft na baada ya hapo niliishia katika mahakama ya Minneapolis na huo ndo ukawa mwanzo na mwisho wa kutuma barua pepe”.

#5. Alikataliwa kujiunga na Chuo Cha Biashara cha Havard

Havard University ni moja katika vyuo mahili sana duniani tena vinasifika kwa utoaji wa elimu bora, Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Nebraska kwa miaka mitatu, Warren Buffet aliamua kutuma maombi ya kujiunga katika Chuo Kikuu Cha Havard katika tawi la biashara.

Alipoitwa katika mahojiano ili kutambuliwa uwezo alionao, ndipo Ofisi ya Biashara Havard ikamwambia kuwa hafai na akate tamaa kujiunga na chuo hiko.

Hata hivyo baada ya kukataliwa katika vyuo vingine vingi Buffet aliamua kujiunga na Chuo Cha Biashara Columbia ambako huko alikutana na Maprofesa Benjamin Graham na  David Dodd ambao walifanikisha kuzifikia ndoto zake.

#6. Hajawahi kubadilisha nyumba ya kuishi tangu mwaka 1958.

Mara nyingi tunaposikia kuwa fulani ni bilionea basi akili yetu huwaza mambo mengi ya kifahari kuhusu mtu huyo, labda atakuwa anaishi katika kasri kubwa la kifalme, ama analmiliki magari mengi ya kifahari.

Hii imekuwa tofauti kwa Warren Buffet kwani yeye bado anaishi katika nyumba yake ya zamani tangu mwaka 1958 iliyoko huko Ohama, nyumba hiyo yenye vyumba 5 vya kulala na vyoo viwili aliinunua kwa gharama ya Dola za kimarekani 31,500.

#7. Watu hulipa mamilioni hili kula chakula cha mchana na Buffet.

Hii inaweza kuwa jambo la kushangaza sana lakini huo ndio ukweli mtu hutoa zaidi ya mamilioni ya fedha hili apate nafasi ya kwenda kushiriki chakula cha mchana na Buffet.

Wapo ambao wamewahi kuweka kiasi cha Dola za Kimarekani  milioni 4.57 ili kuweza kupata chakula cha mchana na Warren Buffet.

#8. Mwaka 2013 aliweza kuingiza Dola Milioni 37 kila siku.

Mwanzoni mwa mwaka 2013 Buffet alikadiriwa kuwa na utajiri wa dola za kimarekani bilioni 46 thamani ya utajiri wake ilipanda mpaka kufikia dola za kimarekani bilioni 59 mwishoni mwa mwaka 2013. fedha hizo zilitokana na kuongezeka kwa thamani ya fedha katika soko la biashara hali ambayo ilimfanya Buffet kuwa na uwezo wa kuingiza dola milioni 37 kila siku.

#9. Buffet anamiliki aina 20 za Suti ambazo hakununua hata moja.

Mfanyabiashara huyo mkongwe anamiliki aina 20 za suti za gharama kubwa, lakini cha kushangaza hakuwahi kununua hata suti moja kati ya hizo!.

Katika jambo hili Buffet aliiuambia mtandao wa CNBC kuwa alipokuwa hotelini katika safari yake kuelekea China Vijana wawili walifika katika chumba chake na kuanza kumfanyia vipimo vya nguo, walipomaliza ndipo wakatoa kitabu kilichojaa michoro mbalimbali ya suti za gharama na kumpatia Buffet na wakamuomba achague moja ambayo ameipenda kisha mwalim wao Madam Lee angeitengeneza kwa ajili yake.

Kabla hata ya kumfahamu mwanamitindo huyo mashuhuri alimaarufu kama Madam Lee kutoka China, Buffet alichagua Suti nzuri ambayo aliona ingemfaa ndipo akatengenezewa na kupatiwa.

Urafiki wa kazi kati ya Madam Lee na Buffet ulizidi kukua kwa kasi huku Madam Lee akizidi kumtumia suti mbalimbali,  baada ya muda Lee alianza kupewa mialiko mpaka kwenye mikutano ya mwisho wa mwaka ya Buffet na huko ndipo akapata pia nafasi ya kutengeneza suti za matajiri wengine kama Bill Gates.

#10. Baba wa Mkewe alimuonya kuwa angeshindwa kufikia malengo yake.

Baada ya Buffet kumuoa mkewe mnamo mwaka 1951, baba mzazi wa mkewe alimuomba Buffet mezani katika mazungumzo, baada ya kumsikiliza Buffet akiwa anaeleza juu ya mipango yake juu ya ndoto zake za kusaka taji ya ubilionea, Baba huyo alimuambia Buffet kuwa hangeweza kufanikiwa katika ndoto hizo.

Hivyo baba mkwe huyo alifikiri kuwa endapo Buffet atashindwa kufikia malengo yake basi mwanye atakuwa akiishi maisha magumu mno, jambo ambalo kwa sasa limebaki kuwa historia tu kwani Buffet hakushindwa katika safari yake ya kusaka utajiri.