Je Wajua kuwa rasta za mwanaharakati wa Jamaica ambaye pia alikuwa mke wa hayati Bob Marley  ziliwahi kuokoa uhai wake?

Jamii ya Rastafari ndio jamii ambayo inaongoza kuwa nywele nyingi kichwani zilizosukwa katika ustadi wa kipekee, jamii inaamini kuwa nywele zao haziruhusiwi kunyolewa katu!.

Mwimbaji maarufu wa Muziki wa Reggae kutoka Jamaica  Alpharita Constantia Anderson  wengi humfahamu kama Rita Marley aliwahi kunusurika kifo baada ya kupigwa risasi kichwani. Mtandao maarufu wa Jamaica Obsever umeripoti kuwa, rasta nyingi alizokuwa nazo mwanamuziki huyo ndizo zilikuwa  msaada katika kuzuia risasi isipenye zaidi mpaka kufikia katika ubongo wake.

Mwanaharakati huyo alizaliwa Julai 25 mwaka 1946 huko  Cuba maeneo ya Santiago, huku harakati za uimbaji wake zikianzia katika ardhi ya Jamaica akiwa mmoja kati ya wanachama wa kundi la I-Threes pamoja na Marcia Griffiths na Judy Mowatt waliojizolea umaarufu kupitia uimbaji wa sauti katika bendi ya Bob Marley (The Wailers).

Kati ya miaka ya 1960, ndipo Rita alipokutana na Bob Marley katika harakati zake za kusaka mwangaza katika tasnia ya muziki, Baada ya Bob Marley kutambua kipaji na sauti nzuri ya muziki iliyojificha kwa Rita.

Ukaribu wao uliongezeka huku Bob Marley akiwa kama msimamizi na mkufunzi wa Rita katika mafunzo ya sauti na uimbaji, Hatimaye ukaribu wao ulizidi hadi kufikia hatua ya wawili hao  kuangukia katika penzi zito.

Wakiwa bado wapenzi Rita akiwa katika kundi la Soulettes walifanikiwa kuachia nyimbo kama vile “Time for Everything”, “ Turn Turn Turn” ambazo walifanikiwa kuziachhia mwaka 1966 ikiwa kama kava ya nyimbo iliyotamba kwa kipindi hiko iliyoitwa  The Byrds, hawakuishia hapo tu bado waliendelea kuachia nyimbo nzuri zilizotamba kama “One More Chance”,  “Friends and Lovers” na “That Aint Right” waliyoshirikiana na kundi la The Wailers .

Baada ya kuachia albamu kadhaa katika tasnia ya Muziki wa Reggae Bob Marley na Ritha Marley walifanikiwa kufunga ndoa Februari 1966.

Ukimzungumzia Rita Marley huwezi kuacha kuzungumza na kipaji cha uandishi alichokibeba mwanamama huyo, katika vitabu vyake viwili ambavyo ni “No Woman No cry” na  “My life with Bob Marley” amevumbua mambo mengi kuhusu maisha yake ikiwemo alivyoanza kulelewa na shangazi yake aliyejulikana kama Viola huko Greenwich Park Road.

Picha kutoka matandaoni, ikimuonesha Rita Marley Mke wa Bob Marley

Mwaka 1976 ulikuwa mwaka wa tabu na majonzi kwa mwanamuziki huyo mkongwe kufuatiwa na tukio la kushambuliwa kwa risasi na watu ambao walishukiwa kuwa ni maadui wa Bob Marley.  Siku mbili kabla ya tamasha la “Smile Jamaica” liliotengenezwa na Bob Marley akishirikiana na Waziri Mkuu wa Jamaica kwa wakati huo, Michael Manley.  Rita, Bob na meneja wao Don Taylor walikumbwa na shambulio lililohusisha matumizi ya silaha za moto.

Mwandishi wa habari wa Daily News Leslie Miles ambaye ndiye aliyekuwa shahidi wa shambulio hilo alisema kuwa “tukio limetokea majira ya saa tatu kamili usiku, limetokea ikiwa Bob Marley na bendi nzima ya The Wailers wakiwa wanafanya maandalizi kwa ajili ya tamasha, baada ya kutimia saa tatu na dakika ishirini usiku walimaliza na kuanza safari, hawakufika mbali niliona gari lingine likiwa kwa mbele limewazuia na watu wake wakiwa nje ya gari wamebeba silaha za moto kisha wakaanza kushambulia.

Katika shambuliio hilo Rita alijeruhiwa na risasi ya kichwa, na meneja Don alipigwa risasi maeneo ya mguuni huku Bob akiwa amejeruhiwa zaidi baada ya kupigwa risasi katika upande wa kulia wa kifua chake.

Baada ya tukio hilo Rita na Bob na wengine waliojeruhuwa katika shambulio hilo walichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha West Indies ambako walipatiwa matibabu na hatimaye kuruhusiwa

Baada ya kupona Bob Marley, Mkewe , The Wailers na I-Three walifunga safari kulekea London, Uingereza. Kwa kipindi hiko Bob Marley alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Cindy Breakspeare mwanamitindo kutoka Jamaica ambaye alitunukiwa taji ya miss world mwaka 1976.