Mwimbaji wa muziki kutoka Nigeria anayefahamika kama Patoranking, amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kutupa shilingi yake kwa mashabiki wa muziki  akiwapa ushauri wa kutengeneza ajira.

Kupitia chapisho lake katika mtandao wa twitter, mwimbaji huyo wa muziki wa reggae pamoja na dance hall, ameandika kuwa “kama huwezi kupata kazi, tengeneza moja”.

Picha kutoka mtandaoni inayoonesha maneno yaliyoandikwa na mwanamuziki Patoranking

Chapisho hilo ameliweka kufuatiwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Nigeria.

Hivi karibuni Legit.ng mtandao maarufu nchini Nigeria umeripoti kuwa Patoranking anamiliki watoto 150 ambao atawasomesha mpaka kufikia Chuo Kikuu.

Chapisho la Patoranking limekuwa gumzo katika mtandao wa twitter baada ya mashabiki kuja juu na kulizungumzia suala la ukosefu wa ajira nchini Nigeria kupitia ukurasa wake.

Ikumbukwe kuwa kabla ya chapisho hili, mwanzo mwanamziki huyo aliweka picha katika ukurasa wake wa twitter kisha akaandika kuwa “Ada ni dola za Kimarekani 15000 kwa mwaka, hivyo sawa na dola za Kimarekani 45000 kwa miaka mitatu. lakini wanafunzi 10 ambao watakuwa chini ya Patoranking Scholarship Program Ni Buree… Mungu ni Mkubwa”

Mtumiaji wa mtandao huo anayetambulika kwa jina la Mark Ogbonnanya alimjibu mwanamziki huyo kwa kumuambia kuwa kama anataka kuanzisha programu za namna hiyo basi aanzie nyumbani kwake kwanza.

Ndipo Nguli huyo anayetamba kwa kibao cha Suh Different alipomjibu shabiki kuwa tayari ana wanafunzi 150 ambao anawasaidia kulipa ada mpaka kufikia chuo kikuu.