NYOTA wa filamu nchini China Jackie Chan, ametangaza kutoa kitita cha fedha Yuan milioni 1(zaidi ya shilingi milioni 300 za kitanzania) kwa mtu au kikundi cha watu ambao wataweza kugundua tiba ya ugonjwa wa Corona.

Virusi vya Corona vimekuwa vikitikisa vichwa vya watu wengi duniani ikiwemo viongozi wa nchi mbalimbali, pia baadhi ya mastaa ambao kwa umoja wao wamekuwa wakiimba nyimbo za maombolezo na kutoa pole kwa waathirika wa virusi hivi.

Jarida ya The straits Times limesema kuwa muigizaji maarufu wa filamu kutoka nchini China, Jackie Chan ametoa kitita cha fedha kiasi cha Yuan milioni 1 ambazo ni zaidi ya milioni 300 za Kitanzania kwa mtu yeyote atakayegundua tiba ya ugonjwa huo.

Nyota huyo kutoka Hong Kong aliweka chapisho lake katika akaunti yake ya Weibo, akieleza kuwa ameguswa kutoa fedha hizo ili kutafuta tiba juu ya ugonjwa huo, ukiachilia mbali nyimbo zinazoimbwa kuwafariji walioathirika na ugonjwa huo.

Katika ukurasa wake wa Weibo Jackie Chan amendika kuwa…

Sayansi na teknolojia ndio ufunguo katika kuwashinda virusi hawa, na ninaamini watu wengi wana mawazo sawa na mimi, katika kutumaini kuwa tiba itapatikana hivi karibuni

nimepata wazo sasa… haijalishi ni mtu ama shirika gani litavumbua kinga ya virusi hivi, nataka kuwashukuru kwa Yuan milioni 1

Nyota huyo wa filamu ya “Rush Hour” aliongeza kwa kusema kuwa hii si kwasababu ya pesa bali, hafurahishwi kuona mitaa ikiwa tupu na watu wake wako njiani wakipambana na ugonjwa huu mpaka kufa, hali walitakiwa wawe wanafurahia maisha yao.

Chapisho lake katika mtandao wa Weibo limepata zaidi ya penda 53000 huku wananchi wakimshukuru na kumpongeza katika utoaji wake pale nchi ya China inapokumbwa na majanga.

Licha ya zawadi hiyo aliyoahidi, wapo wananchi ambao wamekuwa wakimuomba Nyota huyo aongeze kiwango cha fedha hizo hadi Yuan milioni 10.