Ilipoishia….

Kabla ya kufanya hivyo alipewa maagizo ya sehemu ambayo alitakiwa kukaa, baada watu wote kutulia haikuchukua muda mrefu ndege ikapaa juu angani kama ndege tai,

Endelea sasa…

Alihisi kama utani au filamu inaendelea katika maisha yake, alihisi anaota ndoto, alibaki na mawazo tele ndani ya akili yake hakuweza kutambua hata mahali alipokuwa akielekea.

Alijiuliza ni watu gani ana ugomvi nao mpaka waje wamteke na kumpeleka Nigeria, sehemu ambayo hakuwahi kufika kabla, alijiuliza ni kwanini wana fanya hivyo,

Ndege ilikata mawingu kwa kasi mno, moyo wa Ndaki ulienda kasi muda wote, alikosa hata hamu ya kumeza mate, muda wote koo lake limekauka kwa taharuki alizokuwa nazo!

Safari ya ndege kutoka Pewagia kuelekea Nigeria haikuwa ndefu sana hivyo baada ya muda mfupi hatimaye ndege ilitua katika uwanja wa ndege wa Lagos, Nigeria na hapo tayari ilikuwa imeshatimu saa tisa usiku.

Wote walishuka Ndaki aliwaona wavulana wengine ambao alikuwa nao katika ndege  wakiongozana kila mmoja katika kundi lake kisha wakaingia ndani ya magari ya kifahari na kutokomea gizani.

Naye pia hakuwa na budi hila kuwafuata watu ambao ndio wenyeji wake nchini Nigeria walipanda gari kisha na kuondoka.

Baada ya muda walisimama mbele ya geti kubwa la jumba la kifahari, kisha walishuka na kuelekea ndani ya jumba hilo, Ndaki alibaki akishangaa ukubwa wa jumba hilo aliangalia alama alizoziona ndani mule hii ikamfanya kutambua kuwa lilikuwa ni kasri la kifalme, alipiga hatua moja mbele huku pembeni yake akiwa ameshikiliwa na wanaume wawili   na mbele akiongozwa na msichana mmoja aliyemtambua kwa sauti yake.

Walitembea wakivuka milango mikubwa iliyotengenezwa kwa dhahabu halisi, na rangi zenye kuvutia, mbele yake walikuwa wakiulekea mlango mkubwa sana kupita milango yote ndani mule, walipoufikia waliufungua kisha wakaingia ndani.

“Alaaah!!….. Mungu wanguu ni wapi, hapa mahali kama peponi!..” alijisemea moyoni mwake uzuri wa sehemu aliyokanyaga ulimfanya kuwa na hofu kwani alishazoea kijumba chao cha kawaida lakini leo ameingia katika Kasri la kifalme

Aliona ila mtu aliyefuatana naye akiwa anainamisha kichwa chake chini kabla ya kuingia ndani kabisa hii ni ishara ya kutoa heshima kwa watu walioko ndani ilipofika zamu yake hakufanya hivyo kwani imani yake haikumruhusu kutoa heshima za namna hiyo sehemu asioijua.

Walipita katikati ya watu ambao walikuwa wamefunika vichwa vyao kwa kofia za makoti yao, wote walikuwa wamenyoosha mikono yao juu kama wakiabudu Mungu, kwa hesabu ya haraka haraka alitambua wanaweza kuwa zaidi ya watu 300.

alitembea akiwa katikati yao hadi kuelekea mbele kabisa, ambako aliwakuta wenzake wawili wakiwa wamekaa katika viti vizuri vya kumetameta, wakiwa na tabasamu mwanana, Ndaki alijua kuwa nayeye angekaribishwa kukaa kwenye viti hivyo, la hasha haikuwa hivyo.

Alisikia kicheko kilichojawa na kebehi ndani yake, alipogeuka upande wa pili alipigwa na bumbuwazi!! kuona mwanamke mrembo zaidi kupita wote mule ndani, akiwa amevalia mavazi meupe pee!! Huu kichwa chake kikiwa kimevikwa taji ya kifalme yenye pembe saba za shaba, mwanamke huyo alikuwa na mabawa mgongoni mwake.

Licha ya sifa hizo zote bado uzuri wa sura yake haukupotea hata kidogo, Ndaki alibaki na mshangao mkubwa asijue la kufanya alihisi kama yupo mbinguni kutokana na uzuri wa mwanamke yule lakini alihisi kama yupo kuzimu kwani hakutambua hatima ya maisha yake kwa usiku ule.

Mwanamke yule aliinuka kutoka kitini alipoketi kisha akasema kwa madaha,  “come closer Ndaki son of Mr Simba, and kneel before your Queen……” ( sogea karibu Ndaki kijana wa Mzee Simba kisha upige magoti mbele ya malikia wako), Ndaki hakuweza kupinga alisogea karibu na mwanamke yule ambaye tayari alishatambua kuwa ndiye malikia katika kasri lile.

Alisogea kisha akapiga magoti kwa uwoga, hapo watu wote walikuwa kimya, na wale waliomleta wakiwa karibu naye wakimuangalia tu.

“Young boy with whose courage you dare to disgrace your mighty queen?, who rules your ancestors and your fathers….”  (Kijana unatoa kwa nani ujasiri wa kumtia aibu malikia wako mwenye nguvu?, aliyewatawala mababu na mababa zako…) alisema yule Malikia huku akimuangalia Ndaki kwa hasira kali sana, uso wake ulianza kubadilika na macho yake kuwa makali,

Ndaki alibaki kimya huku machozi yakimbubujika kwani aliona ndio mwisho wake umeshakaribia, hakukuwa na msaada wowote upande wake mbele yake alimuona malikia ambaye tayari ameshawaka a hasira kali,

“What wrong have I done to you…..?” ( Ni kosa gani nimefanya kwako..?) aliuliza huku akitowa na machozi.

“Why would you refuse my offering….? (umewezaje kukataa matoleo yangu..?) malikia alimuuliza kwa ukali

“What offerings my lady… why why me… what did I do…oh..!!? (matoleo gani malikia wangu…. Kwanini kwanini mimi…. Nimefanya nini…. Ooh!!?) Ndaki alijibu huku akiwa katika uoga na hali ya sintofahamu, kwani hakuwa ametambua ni matoleo gani amepewa kisha akakataa.

“Silence! Your mighty queen has no mercy to whoever disgraces her… the rules are rules and the punishment will follow onward upon any creature that dares to abuse me,” (Kimya! malikia wenu mwenye nguvu hana msamaha kwa yeyote anayemtia aibu… sheria ni sheria na adhabu itafuata kwa kiumbe awaye yeyote mwenye kuthubutu kunitukana mimi,) Malikia aliongea kwa hamaki kisha akaendelea……

“See mortal’s young boy, you have insulted my power beyond comprehensions, your mistake don’t deserve mercy So you will visit the hell tonight……… Get rid of him immediately, remember I am thirsty for his blood!!” (ona mwanadamu, kijana mdogo umenitukana nguvu zangu kupita maelezo, kosa lako halihitaji huruma, hivyo utatembelea kuzimu usiku wa leo……. ashughulikiwe sasa hivi, Kumbukeni nina kiu na damu yake!!) Malikia alitoa amri kushughulikiwa kwa Ndaki.

Umati wote uliinama wakionesha ishara ya kukubaliana na Malikia wao, hakuna yeyote ambaye angeweza kupinga na kumsaidia Ndaki, Masikini!! Moyo wake ulienda mbio pale alipoona mazingira yanaandalikwa kwa ajili ya uhai wake kutolewa kafara.

Hakuwai kuwaza hata siku moja kama angeishia kutolewa kafara mbele watu wasiokuwa na huruma, aliona jambia kubwa lililonolewa pande mbili likiletwa mahali pale, mpini wake ukiwa ni wa shaba na makali yake yenye rangi ya udhurungi, kisha aliona chombo kikubwa alifahamu fika kuwa ni kwa ajili ya kuwekea damu yake itakayokuwa ikimwagika huku anakata uhai.

Alisali sala zake za mwisho kisha kisha alimuangalia malikia  ambaye kwa sasa alikuwa na kiu ya kuonja damu yake, kisha akamuangalia msichana  aliyeushika Jambia kwa huzuni huku akikumbuka safari waliyoianza pamoja kutoka nchini kwao Pewagia mpaka kufika Nigeria hakutegemea kama huyo mtu ndiye atakayeondoa uhai wake.

Alifumba macho na kusubiri hukumu yake, kwa mara ya kwanza katika safari yake, alimkumbuka mama yake mzazi Bi Fatma Simba aliishia kumuaga kimoyo moyo tu, “Kwaheri mama yangu kipenzi naamini tutaonana tena” alisikia sauti ya Jambia likinuulia tayari kuondoa shingo yake.

Alituliza mapigo ya moyo wake kimya hili asihisi maumivu yoyote japo woga na hofu vilisukuma machozi kwa wingi machoni mwake .

Bila ya huruma msichana yule aliinua jambia na kulishusha kwa nguvu zote shingoni …… Fyaaaaa!!!…..

MAMAAAAAAA……!! Ndaki alitoa sauti kali iliyopenya mpaka chumbani mwa mama yake… aaaaaah nakufaaa … nakufaaaa!! Nakufaa mama yangu!! Alifumbua macho na kujikuta chini sakafuni purukushani zimemfanya kuanguka kutoka kitandani pake…..

Alaaaas!!! Nilikuwa naota oooh…. Asante Mungu ni heri nimeota tu ni heri haijawa kweli  aaah lakini kwanini ndoto mbaya hivi mmh bila shaka kuna jambo baya linakuja mmh Mungu epushia mbali…

Itaendelea……..