Ilikuwa ni usiku wa sita, dunia imegubikwa na kiza kinene, dalili za mvua zilionekana kwa mbali huku mirindimo ya radi na karatasi zilizopeperushwa kwa upepo mwanana zikiwa ndio wimbo wenye kutia hofu katika mioyo ya watu ambao walikuwa hawajalala usiku huo.

Panya na viumbe wengine wadogo wadogo wakipita katika mitaa ya Arizona wakitafuta mabaki ya chakula hili kuikamilisha siku yao, Ghafla harakati za kutafuta ridhiki yao ilikatishwa na mlio wa tairi za gari moja la kifahari lililokatisha kasi katika barabara zamtaa huo.

Baada ya muda gari hilo liliacha barabara kuu na kusogea pembeni kisha likasimama ndipo waliposhuka watu watatu waliovalia nguo nyeusi tupu na kufunika nyuso zao kwa kofia nyeusi.

Paaaaa!!! Ndaki alishtushwa kutoka usingizini na sauti ya mlango wa chumba chake, huku akiwa amekumbwa na hofu,  akilini mwake aliwaza kuwa majambazi wamevamia chumba chake, hakutaka kupiga kelele kwani alitambua kufanya hivyo kungegharimu usalama wake zaidi.

Alitulia kimya, akiwaza na kuwazua nini cha kufanya kijasho chembamba kilichuruzika kama maji mwilini mwake alihisi mwisho wake umefika!.

Ghafla taa ya chumbani mwake iliwashwa, alipoangalia mbele alitahamaki kuona watu watatu wamesimama karibu yake huku mlango wa chumba  chake ukiwa umevunjwa,  hofu yake iliongezeka mara dufu.

Aliwatazama kwa makini watu wale ndipo alipong’amua kuwa mmoja wao alikuwa wakike, na wawili walikuwa wakiume, wote hao walivalia  nguo nadhifu zenye rangi nyeusi na kofia ambazo ziliziba nyuso zao hivyo Ndaki hakufanikiwa kutambua nyuso zao, lakini aliweza kuona midomo yao tu.

Akiwa katika harakati zake kuwachunguza watu ambao alidhania kuwa ni majambazi ghafla yule msichana alimsogelea kisha akamshika kichwa katika sehemu ya utosi wake na kufumba macho, alifanya hivyo kwa sekunde kadhaa huku Ndaki akiwa ametulia na hakujua la kufanya, akili yake ilijawa na maswali mengi sana hakujua watu hawa ni akina nani.

Baada ya muda wa sekunde kadhaa msichana yule alifumbua macho yake huku yakiwa yamebadilika, yalianza kutoa mwanga wenye rangi nyekundu mithili ya moto mkali wa Jehanam, tayari alionekana kuwa amepata kile alichokitaka.

“He is the right boy that our Queen needs, send him to the car right now!” (Ndiye mvulana sahihi ambaye anahitajika na Malikia wetu, mpelekeni ndani ya gari sasa hivi.) Alisema yule msichana, ambaye kwa wakati huo alionekana kumuachia Ndaki na kuruhusu achukuliwe kupelekwa nje, ndani ya gari.

Ndaki akiwa katika taharuki!! Alishangazwa na lugha iliyotumiwa na watekaji walioko mbele yake, kwani kutokana na shughuli anazofanya alijua wazi kuwa haziwezi kumkutanisha na watu wenye kuongea kingereza kizuri namna hile tena chenye lafudhi ya watu wa Nigeria, alishazoea kuwasikia rafiki zake wakina Kelvin ambao kingereza chao hakikuwa kizuri sana.

Akiwa amezama katika dimbwi la mawazo juu ya ni akina nani hasa wamekuja kumteka usiku ule, aliona wanaume wawili wenye miraba minne wakija na kuhitaji kumkamata, Ndaki aliona sasa wasaa wa kujitetea umefika na akifanya mchezo anaweza kutoweka kama vile walivyotoweka baadhi ya vigogo jijini Dar es salaam.

Alikamata rungu lake tayari kwa shari yoyote itakayojitokeza, ghafla akiwa anajiandaa kurusha rungu lake alianza kuhisi maumivu makali ndani ya mwili wake, maumivu ambayo yalimfanya ahairishe njama zake za kujitetea na kubaki akipiga kelele tu.

Hakuna aliyejali kelele zake, walimbeba mpaka nje kisha wakamuingiza ndani ya gari moja la kifahari lilifungwa vioo vyenye rangi nyeusi, na wakaondoka nae.

Safari yao ilisindikizwa na mvua ya rasharasha, ndani ya gari ni Ndaki pekee aliyekuwa akilalama kwa maswali ambayo hakufanikiwa kupata majibu yake huku machozi yakimtoka alijaribu kuuliza ni wapi anapelekwa lakini hakuna jibu alilopewa.

Safari ilikoma walipofika uwanja wa ndege wa Jamhuri ya watu wa Pewagia, walishuka kisha wakamuarisha Ndaki kushuka, hakuwa na namna ilibidi ashuke kwani ilimpasa kufuata maagizo aliyopewa kwa kuogopa kuingia katika matatizo zaidi,

“We take the private jet and fly to Nigeria….” (tunapanda ndege  kuelekea Nigeria..) Alisema yule msichana. Ndaki aliisikia sauti hii barabara kabisaa, alianza kutambua uzuri alionao msichana yule kupitia sauti japo hakuweza kuona sura ya kamili.

“Mawazo gani haya nawaza nikiwa katika hali mbaya kiasi hiki” Ndaki alijisemea moyoni mwake mwenyewe, alimrishwa kuwafuata watu wale huku yule msichana yule akiwa mbele yao anawaongoza kuelekea katika ndege waliyotakiwa kupanda.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kupanda ndege, hakuwahi kabisa hapo awali hivyo ilikuwa ngumu kidogo kufahamu taratibu za kwenye ndege wakati huo tayari hofu yake ilikuwa imeshaanmza kutulia na hali ya kawaida ilishamjia

Alishakata tama liwalo na liwe huko aendako “Mwanaume hafi kwa usiku mmoja” ndio msemo wa kishujaa uliotawala akili yake kwa wakati huo.

Alipoingia ndani ya ndege, alishangazwa kukuta watu wengine kama yeye, jambo ambalo hakutegemea  aliona vijana wawili wa makamo yake wao pia wakiwa na watu wao watatu kama ilivyokuwa kwake.

Hali hii ilimfanya apunguze uoga kidogo baada ya kuona nyuso za vijana wenzake zikiwa zenye furaha tupu, alitamani kuwauliza kama wanafahamu lolote kuhusu wapi walikuwa wanapelekwa.

Kabla ya kufanya hivyo alipewa maagizo ya sehemu ambayo alitakiwa kukaa, baada watu wote kutulia haikuchukua muda mrefu ndege ikapaa juu angani kama ndege tai,

Itaendelea…….